Wananchi wanaotumia usafiri wa dala dala na magari yaendayo vijijini wametakiwa kuchukua hatua za kuripoti katika vituo vya Polisi au Idara ya Usafiri na leseni mara moja dhidi ya Madereva au Matingo wanaowafanyia vitendo vinavyokiuka sheria za bara barani.

Hatua ya kukomesha vitendo hivyo kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria wahusika hao zitafanikiwa vyema endapo Wananchi watakubali kutoa ushirikiano unaofaa kwa Taasisi hizo katika kukabiliana na usumbufu huo.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akizindua rasmi Wiki ya Usalama Bara barani hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Salama uliopo Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif aliliamuru Jeshi la Polisi, Kikosi cha usalama bara barani kusimamia sheria za usalama bara barani na kuondoa muhali kwa wote wanaokiuka sheria hizo kwa kuwachukuliwa hatua kali za kisheria kwani hakuna mtu aliyekuwa juu ya sheria.

Alisema kwa kuwa suala la usalama wa bara barani linahitaji nguvu za pamoja madereva wana wajibu wa kuwajali watumiaji wengine wa bara bara ikiwa ni pamoja na watembeao kwa miguu, wapanda baskeli wakiwemo pia watu wenye mahitaji maalum.

Balozi Seif alielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya madereva na Matingo wao kuwanyanyasa wananchi ambao ndio abiria wao kwa kutowafikisha mwisho wa safari kama walivyoomba ruhusa ya usafirishaji pamoja na kuwatolea lugha chafu.

Akizungumzia suala la matumizi mabaya ya bara bara Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema bara bara nyingi zinaharibiwa kwa kuwekwa matuta na wananchi baaba ya kukosa imani ya uendeshaji mbovu unaofanywa na baadhi ya madereva.

Balozi Seif alionya kwamba wakati umefika kwa Taasisi inayosimamia masuala ya Leseni kuweka utaratibu wa kuwanyang’anya Leseni Madereva wanaosababisha ajali za mara kwa mara kwa makusudi na uzembe.

Aliitaja sababu moja kubwa inayochangia ajali za mara kwa mara kwenye bara bara nyingi hapa nchini kuwa ni matumizi ya simu za mkononi hali inayomfanya Dereva kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja.

“ Haiwezekani kuchanganya mambo mawili kwa wakati mmoja. Na hili tumekuwa tukilishuhudia pia ndani ya majengo ya ibada ambapo muumini anashindwa kuzima simu yake wakati tayari mlangoni pameshawekwa tangazo la kukumbusha jambo hilo “. Alifafanua Balozi Seif.

“ Ukweli usiofichika ni kwamba Jamii kubwa ya Wazanzibari imekuwa kaidi katika kutii sheria ambazo zimetungwa maalum kwa lengo la kufuatwa uadilifu utakaotoa haki kwa kila Mtu “. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akigusia tukio la uzinduzi wa wiki ya usalama bara barani ikiwa ni sehemu ya kutathmini utekelezaji wa mpango wa miaka kumi ya usalama bara barani ulioanzishwa na Rais wa Zanzibar Dr. Sheni Disemba mwaka 2011 Balozi Seif alisema ajali za bara barani zimefikia kushika nafasi ya Pili kwa kusababisha vifo vingi baada ya ugonjwa wa ukimwi.

Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba uelewa wa hali ya usalama bara barani duniani umeongezeka baada ya shirika la Afya Ulimwenguni { WHO } kueleza kuwa watu wapatao Milioni 1.3 hufa na wengine wapatao Milioni 50 hujeruhiwa ulimwenguni kila mwaka.

Alieleza kwamba ajali ya bara barani zina athari kiuchumi kwa kupunguza nguvu kazi ya Taifa sambamba na kuwaacha watu wenye ulemavu ambao kwa kiasi kikubwa hupunguza uwezo wao wa uzalishaji mali katika kujipatia kipato kinachowawezesha katika maisha yao ya kila siku.

Balozi Seif alisema katika kukabiliana na changa moto hiyo ya ajali za bara barani Serikali itahakikisha inasimamia vilivyo bara bara zinazojengwa ili zikidhi viwango ikiwa ni pamoja na uimara wa bara bara zenyewe, upana, pamoja na kuwekwa kwa alama za bara barani.

Mapema Kamishna wa Polisi Zanzibar Bwana Mussa Ali Mussa alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuchukuwa hatua mbali mbali ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu wa magari pamoja na madereva wazembe.

Kamishna Mussa alisema ajali za bara barani kwa mwaka 2012 zilifikia 855 ikilinganishwa na ajali 849 kwa mwaka 2011 ikiwa na ongezeko la ajali sita wakati ambapo ajali hizo zimesababisha vifo vya watu 138 kwa mwaka 2012 kukiwa na ongezeko la vifo vya watu 47 ikilinganishwa na vile vya mwaka 2011 vya watu 117.

Bwana Mussa alizishauri Taasisi zinazohusika kuweka viwango maalum vya uingizaji wa magari nchini kupunguza vyombo vilivyochakaa ambavyo ndivyo vinavyochangia kuongezeka kwa msongamano wa ajali zinazotokea Nchini.

Kamishna Mussa alisisitiza umuhimu wa kutumiwa kwa utatu ambao ni mawasiliano, mashirikiano pamoja na Uratibu katika kufanikisha malengo ya matumizi bora ya sheria ikiwemo suala la matumizi sahihi ya bara bara.

Wakitoa mawazo yao baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya wiki ya usalama bara barani walisema ajali zinaweza kupungua au kuondoka kabisa iwapo alama za bara barani zitatumiwa kama zilivyokusudiwa.

Walisema wakati busara inaweza kuokoa ajali kwa suala hili kuwekwa katika vichwa vya madereva wakati umefika kwa Wizara ya Maiundo mbinu na mawasiliano kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kulijadili tatizo la matumizi ya simu unaofanywa na madereva wakati wanapoendesha gari bara barani.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top