Tabia ya kuendeleza tamaa iliyosheheni ndani ya vichwa vya baadhi ya Wazazi ya kuwaozesha waume watoto wao wa Kike wakiwa bado wanaendelea na masomo yao inapaswa kuachwa mara moja ili kujengewa ustawi bora watoto hao kwa maisha yao ya baadaye.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Jengo la Skuli mpya ya Shehia ya Shidi Jimbo la Mkanyageni Mkoa kusini pemba wakati akizungumza na Wazazi, Walimu na wanafunzi wanaoishi katika eneo hilo.

Balozi Seif akionyesha furaha yake kutokana na juhudi kubwa zilizochukuliwa na Wananchi wa shehia hiyo za kujiletea maendeleo ya Elimu kwa ujenzi wa Skuli hiyo alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuendelea kufanya na baadhi ya wazazi inachangia kuviza maendeleo ya familia na hata Taifa kwa ujumla.

Alisema bado jamii inapaswa kuendelea kuwekeza katika Sekta hii muhimu ya Elimu sambamba na wazazi kufuatilia nyendo za watoto wao kwa lengo la kuhakikisha kizazi hicho kinajengewa mazingira madhubuti ya kuja kutoa huduma kwa wananchi katika njia ya Kitaalamu.

“ Huu ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na wana Shidi katika kuwajengea mazingira mazuri ya kielimu watoto wao na ni vyema mkajitahidi zaidi katika miradi ya maendeleo ambayo haihusiani na itikadi za kisiasa”. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewapongeza wananchi hao wa Shehia ya Shidi kwa uwamuzi wao wa kujisogezea miradi muhimu ya maendeleo na katika kuunga mkono juhudi hizo ameahidi kusaidia Bati hamsini kuungana na wale waliojitolewa kuchangia ujenzi huo ili kukamilisha kiwango kamili kinachohitajika katika uwezekaji wa Skuli hiyo.

Ameishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kufikiria kutoa upendeleo Maalum kwa Jengo hilo jipya ambalo kukamilika kwake kutawaondoshea usumbufu watoto wa kijiji hicho wanaolazimika kuvuka kwa kufuata elimu masafa marefu.

“ Tunaelewa jukumu kubwa lililonalo Wizara ya Elimu katika kukamilisha Majengo ya Skuli yaliyojengwa na Wananchi wenyewe kwa njia ya kujitolea lakini wanapaswa kulifumbia macho hili la Shidi kutokana na uzito wake”. Alifafanua Balozi Seif.

“ Zipo skuli nyingi hapa nchini ambazo zinaendelea kujioongeza majengo mengine mapya kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ongezeko la watoto wao. Lakini hili la Shidi jipya na ndio kwanza wameanza kuanzisha skuli sasa Wizara ya Elimu inapaswa kuliona hili”. Aliongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Akimkaribisha Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Kanal Mstaafu Juma Kassim Tindwa alisema Wananchi wa Shehia ya Shidi hawajakosea kuwekeza katika Sekta ya Elimu kwani haypo ndio miongoni mwa malengo makubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Katika Risala yao wananchi hao wa Kijiji cha Shidi Wilaya ya Mkoani ambayo iliosomwa na Mwalimu Rajab Abdulla Tamim alisema chimbuko la ujenzi wa Skuli hiyo limetokana na Jumuiya ya Mazingira ya Mimka kwa kuwamua kutoa changamoto ya mifuko kumi ya saruji kwa wananachi hao.

Mwalimu Rajab alisema wananchi wa Shidi walifikia kuhamasika na kuanza harakati za ujenzi mwaka 2004 ambapo hadi sasa likifikia hatua ya kukamilika kwa linta jingo hilo limeshafikia gharama ya zaidi ya shilingi milioni 10.6.

Watoto wa Kijiji cha Shidi kiliopo Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba hivi sasa wanalazimika kufuata elimu zaidi ya masafa ya kilomita mbili na tatu katika skuli za Ng’ombeni na Mkanyageni hali ambayo inaleta usumbufu kwa wale wanaoanza darasa la kwanza.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top