Wanavikundi vya ushirika wanaojishughulisha na kazi za amali nchini wanapaswa kuzingatia fani yao katika dhana nzima ya kujipatia ajira badala ya tabia ya kufikiria ajira hupatikana Serikalini pekee.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati akiyafunga mafunzo ya miezi sita ya ukataji nguo katika Fani ya Ushoni kwa Kikundi cha Ushirika cha Hatubaguani cha Jimbo la Kitope hafla iliyofanyika hapo Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “ B “.

Mama Asha alisema Ushoni ni miongoni mwa kazi pekee inayotoa ajira ya uhakika hasa kwa vikundi vya ushirika. Hivyo wanavikundi hao wana wajibu wa kuhakikisha mafunzo yao wanayaendeleza lengo likiwa kujiongezea mapato sambamba na kusaidia Familia.

Alisema zipo familia na vikundi vinavyoendesha maisha yao kwa kutegemea sekta ya ushoni na matokeo yake familia hizo zimekuwa zikiendesha maisha yao bila ya kutetereka.

“ Tumeshuhudia baadhi ya Familia zimekuwa zikiyakabili matatizo yao yanayowazunguuka bila ya msaada wa utegemezi wa waume zao jambo ambalo limekuwa faraja kwao pamoja na watoto wao”. Alisisitiza Mama Asha.

Aliwalaumu baadhi ya wanachama wa Kikundi hicho cha Hatubaguani waliokuwa na tabia za kupangilia ushiriki wa mafunzo yao jambo ambalo litasababisha kuwavunja moyo Viongozi waliojitolea kudhamini mafunzo hayo.

Alisema walimu na Viongozi wa Jimbo hilo walijitolea kwa hali na mali kuhakikisha mafunzo hayo ya ushoni yanaendelea na kuleta tija ya kutoa ajira kwa wana kikundi hicho.

Katika kuunga mkono harakati za mafunzo hayo Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alikabidhi mchango wa Shilingi Laki Tano Taslim { 500,000/- } kusaidia gharama za ufundishaji wa wana kikundi hicho.

Akitoa nasaha zake Mkurugenzi wa Chuo cha Ushoni kiliopo Magomeni Mjini Zanzibar { Modern Tailoring Academy } ambacho ndicho kilichosimamia kuendesha mafunzo hayo Mwalimu Rashid Makame Shamsi aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Kitope kwa hatua zake za kuwajengea uwezo wa ajira wananchi wake.

Nd. Rashid alisema Uongozi huo umeonyesha moyo wa kuwatafutia ujuzi Wana Kikundi hao na katika kuunga mkono juhudi hizo aliahidi kwamba Uongozi wa Chuo chake utakuwa tayari kuwaendeleza tena wana kikundi hao kwa hatua ya Pili na ya tatu endapo utaratibu wa mafunzo hayo utaandaliwa.

Mapema Mwenyekiti wa Kikundi cha Hatubaguani Bibi Sichana Said Haji amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi kwa moyo wake wa kujitolea kusimamia uanzishwaji wa mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kujipatia ajira ya kudumu.

Bibi Sichana kwa niaba ya wana kikundi wenzake wameahidi kwamba mafunzo waliyoyapata ya miezi sita yakijumuisha wanafunzi 30 watayatumia vyema kwa manufaa yao na vizazi vyao.

Hata hivyo wanafunzi waliofanya mtihani wao ambapo wanatarajiwa kupatiwa vyeti vya Modern Tailoring Academy walikuwa 17 kati ya 30 na kufikia asilimia 50% ya wanafunzi hao.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top