Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Hani Mominah akimkabidhi Boksi mbili za zawadi za Misahafu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo nyumbani kwake Mtaa wa Haile Sellassie Jijini Dr es salaam.
Saudi Arabia iko tayari kutoa fursa maalum kwa walimu wa Zanzibar kwa kupata taaluma zaidi ya elimu ya Dini na lugha ya Kiarabu Nchini humo kwa lengo la kuwajengea uwezo wa ufundishaji.

Fursa hiyo imetolewa na Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Hani Mominah wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Nyumbani kwake Mtaa wa Haile Sellassie Mjini Dar es salaam.

Balozi Hani Mominah ambae alifika kwa Balozi Seif kumuaga rasmi baada ya kumaliza utumishi wake Nchini Tanzania alisema fursa hizo zitahusisha mafunzo kati ya vipindi vya miezi Minne, Sita na Mwaka Mmoja.

Alisema cha msingi na kuzingatiwa zaidi ni suala la mawasiliano kati ya pande hizo mbili ili kuandaliwa utaratibu wa mfumo wa kuityumia vyema fursa hiyo muhimu.

“ Sioni kama vipo vikwazo vyovyote katika suala hili kwani hivi sasa tayari wapo wanafunzi wapatao 40 wa Tanzania wanaopata mafunzo ya Dini na Lugha ya Kiarabu Nchini Saudi Arabia katika vyuo Vikuu tofauti”. Alifafanua Balozi Hani Mominah.

Akizungumzia ibada kubwa ya Hijja inayofanyika Macca Nchini humo Balozi Hani alisema Serikali ya Nchi hiyo inajitahidi kuimarisha miundo mbinu ya kisasa katika kuwahakikishia waumini wa Dini ya Kiislamu ulimwenguni wanakwenda kutekeleza ibada yao ya Hija kwa utaratibu muwafaka.

Balozi Hani alifahamisha kwamba hatua hizo zimekuja kufuatia kuongezeka kwa idadi kubwa ya waumini wa dini hiyo wanaokwenda kutekeleza nguzo hiyo ya tano ya Kiislamu.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Saudi Arabia kwa hatua zake za kusaidia Mawendeleo ya Zanzibar katika sekta ya Elimu na Dini.

Balozi Seif alisema Saudi Arabia imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kupitia Mfuko wake wa Misaada ya Kimataikfa { Saud Fund } ambao umewezesha kunyanyua kiwango cha Elimu ya Dini ya Kiislamu Nchini.

Licha ya juhudi hizo Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar bado ina nkiwango kidogo cha walimu wa masomo ya Dini na Kiarabu hasa ikilinganishwa na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi maskulini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiomba Saudi Arabia kupitia Balozi wake huyo Bwa Hani kuangalia uwezekano wa kusaidia katika sekta ya maji ambayo ni muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanaadamu.

Balozi Seif alisema licha ya juhudi kubwa iliyochukuliwa na Serikali kwakushirikiana na nguvu za wahisani lakini bado Mji wa Zanzibar unaendelea kukumbwa na huduma ya maji safi na salama katika maeneo yake mengi.

Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Hani Mominah amemaliza muda wake wa utumishi wa mwaka mmoja akiwakilisha Nchi yake hapa Tanzania.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top