Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar imezuia ujenzi unaoendelea wa sehemu ya wazi ambayo pia hutumiwa na wananchi wa eneo hilo kama njia ya wazi ya kupita ambao unafanywa na Uongozi wa Hoteli ya Pack iliyopo kinu cha Taa Malindi Mjini Zanzibar.

Uzuiaji Ujenzi huo umekuja baada ya Mmiliki wa Hoteli hiyo kuendeleza ujenzi bila ya kupata kibali sambamba na kukiuka taratibu za matumizi ya eneo hilo ambazo zimewekwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Mji Mkongwe kuwa ni eneo la wazi { Public Areas } kwa ajili ya Wananchi wote.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe Ndugu Said Sarboko Makarani alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye alifika kukagua eneo hilo kwamba mmiliki huyo tayari ameshaandikiwa Barua rasmi ya kuzuia ujenzi wowote lakini anaonekana kukaidi agizo hilo la Mamlaka.

Ndugu Sarboko alisema eneo hilo kwa mujibu wa ramani ya Miji mkongwe limekuwa na mtaro wa asili unaopitishia maji machafu kuelekea Baharini. Hivyo ujenzi huo unaweza kuathiri kwa asilimia kubwa matatizo ya mafuriko ya maji machafu katika eneo hilo.

Alimueleza Balozi Seif kwamba Mmiliki wa Hoteli hiyo alishauriwa mapema kutolitumia eneo hilo la wazi kwa ujenzi wa aina yoyote ambalo liko pembezoni mwa jengo lake kwa kuhofiwa kuvuruga mipango Miji pamoja na kusumbuwa Wananchi wanakusudia kupita njia hiyo.

“ Tumeshamuarifu kuacha ujenzi kila mara lakini kinachoonekana mjenzi huyu hutumia mwanya wa kuendeleza ujenzi huo anapogundua kwamba sisi wasimamizi tuko nje ya Nchi. Tunaamini anatabia ya kutufuatilia nyendo zetu maana muda mfupi tu kama hatupo anautumia kukamilisha azma yake hiyo”. Alisisitiza Nd. Said Sarboko Makarani.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati agizo la kuzuia ujenzi huo likiendelea aliuagiza Uongozi wa Mmlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, Taasisi ya Ardhi na Mipango Miji kumwita Mmiliki wa Hoteli hiyo ili kumkumbusha zaidi mfumo wa muendelezo wa Mamlaka ya hifadhi ya Mji Mkongwe na taratibu zake.

“ Hakikisheni kwamba maamuzi yenu yote mtakayoyatoa mara baada ya kukutana na Mmiliki huyo mnaniletea mara moja Ofisini kwangu”. Aliagiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif alionya kwamba bado wapo baadhi ya watu wanaoendelea kukaidi maagizo, ushauri na hata amri zinazotolewa na Serikali na taasisi zake kwenye masuala mbali mbali yenye kukiuka utaratibu zilizowekwa.

Alisema hali hiyo baadaye hugeuzwa na watu hao kuwa kama unyanyaswaji unaoelekezwa katika dhana ya misingi ya kukiukwa kwa haki za Binaadamu jambo ambalo kamwe Serikali Kuu halitalikubali na kuliridhia.

“ Wapo Watu tayari wameshajijengea tabia ya kudharau maagizo na amri halali za Serikali kwa kisingizio cha haki za Binaadamu na zinapochukuliwa hatua wanakuwa walalamikaji wakubwa dhidi ya Serikali”. Alielezea Balozi Seif.

“ Mwaka jana wakati nilipokuja kufungua Mkutano wa uchaguzi wa Umoja wa Vijana, nilipomaliza nilikuja kukagua hatua za ujenzi wa Hoteli hii hapa na kuagiza mmiliki huyu aheshimu eneo la wazi kwa ajili ya shughuli za Wananchi. Sasa hili halikutekelezwa na ujenzi unaendelea. Maana yake nini ?”. Alihoji Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kukumbusha kwamba Jamii lazima iheshimu maamuzi ya Serikali hasa katika suala la matumizi sahihi ya Ardhi na wakielewa kwamba Ardhi yote inaendelea kuwa mali ya Serikali.

Balozi Seif alifafanua kwamba Serikali wakati wowote inaweza kuamua ifanye nini katika matumizi ya ardhi hiyo hata kama yupo Mtu aliyepewa kwa matumizi yake ya kawaida iwe kilimo, Makazi na hata kama harakati za Kiuchumi na Kibiashara.

Othmana Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top