Wananchi wa Kijiji cha Kipandoni Wadi ya Upenja wanatarajiwa kufaidika na huduma za maji safi katika kipindi kifupi kijacho mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa tangi lao la kuhifadhia maji yakiwemo marekebisho madogo madogo ya mabomba.

Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Wananchi hao wakati alipopata fursa yakukagua ujenzi wa Tangi hilo ambao ulikuwa na hitilafu zilizopelekea kuchelewa kukamilika kwa mradi huo katika wakati uliopangwa.

Balozi Seif alisema katika kuhakikisha mradi huo unakamilika na kutoa huduma aliahidi kuchangia shilingi Milioni mbili { 2,000,000/- } ili kusaidia kukamilishia ujenzi huo sambamba na mifereji itakayotoa huduma kwa wananchi hao.

Alisema Wananchi wanapaswa kuwa na uhakika wa kupata huduma za maji safi na salama ili muda wanaoutumia kutafuta huduma hiyo waweze kuuelekea katika harakati za kujitafutia maendeleo.

“ Katika kuona tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu nimefikia maamuzi ya kuahidi kutoa shilingi milioni 2,000,000/- ili kukamilisha mradi huo wa maji safi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ujao”. Balozi Seif aliwaahidi wananchi hao.

Mbunge huyo wa jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliangalia mradi wa maji safi wa Kiwengwa na kuutaka Uongozi wa Shehia hiyo kufanya mawasiliano na Uongozi wa Hoteli ya Melia ili kuondosha hitilafu zilizojitokeza katika matumizi ya umeme unatumiwa kwenye kisima cha mradi huo wa maji.

Balozi Seif aliyepata fursa ya kuangalia chanzo cha hitilafu hiyo alisema bado hakujawa na sababu ya kuendeleza mvutano huo baada ya kupokea na kupima maelezo yaliyotolewa kutoka pande zote mbili.

“ Nimeshazungumza na Uongozi wa Hoteli ya Melia na kunieleza kwamba hauna matatizo yoyote na wana kijiji hao lakini kilichojitokeza ni ule uamuzi wa wana Kijiji hao kuchukuwa hatua ya kuunga umeme bila ya kuuarifu uongozi wa Hoteli hiyo”. Alifafanua balozi Seif.

Akizungumza na Wana vikundi vya ushirika wa Kufuli tatu wa Vijiji vya Kipandoni na Kiwengwa mara baada ya kuvifungua visanduku na kugawa faida kwa wanachama wake Balozi Seif amewapongeza wana vikundi hao kwa uamuzi wao wa kuendeleza ushirika wa aina hiyo.

Alisema ushirika huo ambao huondosha lawama ya kuwepo kwa dhana ya ubabaishwaji na utapeli kwa baadhi ya waliopewa dhamana unaonekana kuwa na mwanzo mzuri wa mafanikio kwa wanachama wake.

Katika kuunga mkono Vikundi hivyo Balozi Seif Ali Iddi amekabidhi mchango wa shilingi laki mbili kwa kila Kikundi kati ya Vikundi vinane vya Vijiji vya Kipandoni na Kiwengwa ili kuviongezea uhimili wake.

Mbunge huyo pia alikagua eneo linalojengwa Skuli ya Msingi ya Kiwengwa Cairo ambalo wananchi wa Kijiji hicho wamemlalamikia ufinyu wa eneo hilo kufuatia baadhi ya watu kuendeleza ujenzi wa makaazi baada ya kukatiwa hati miliki ya viwanja kutoka kwa mamlaka zinazohusika.

Halkadhalika Mbunge huyo aliwapongeza Wanafunzi wa Skuli ya Kiwengwa Kumba urembo waliofanya mitihani yao mwaka uliopita ambapo jumla ya wanafunzi 25 kati ya 29 wamefaulu vyema mitihani yao.

“ Nakuhakikishieni wanangu kwamba ule utaratibu tuliojipangia wa kuwazawadia wanafunzi wetu upo na tukijaaliwa tutautekeleza katika kipindi kipidi sio kirefu sana”. Alisema Balozi Seif.

Akizungumza na wanachama wa Matawi ya CCM ya Kipandoni na Kumbaurembo Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM amewataka Wanachama watakaopata fursa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa mabaraza ya Katiba ya Wilaya wahakikishe kwamba wanazingatia matakwa yaliyotolewa na wananchi wakati wa kutoa maoni yao.

Alisema Tume ya mabadiliko ya Katiba itatengeneza rasimu itakayowasilishwa katika mabaraza hayo ya Katiba ya wilaya ili yapate kujadiliwa na kupata rasimu iliyokamilisha ushiriki wa wananchi walio wengi zaidi.

“ Wapo baadhi ya watu waliojaribu kutaka kuingiza vipengele vya mfumo wa Katiba visivyo na maslahi mema ya muelekeo wa katiba mpya ya muungano unaotakiwa”. Alieleza Balozi Seif.

Zaidi ya Shilingi Milioni mbili zimetolewa na Mbunge huyo katika ziara hiyo ikiwemo pia shilingi Laki mbili zilizotolewa na Mke wa Mbunge huyo Mama Asha Suleiman Iddi kuchangia kifusi, mchanga na saruji kwa ajili uendelezaji wa Tawi la CCM la Kipandoni.

Othman Khamis Ame

0 comments:

 
Top