Benki za Biashara Nchini zimetakiwa kuzingatia mahitaji ya wananchi katika kuchukuwa sarafu na noti zenye kuleta uwiano kwenye matumizi ya kibiashara. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito huo katika hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Benki Kuu cha kutunzia na kusambazia sarafu katika Benki ya Watu wa Zanzibar { PBZ } Tawi la Chake chake Pemba. 

Balozi Seif alisema yapo mafanikio miongoni mwa Wananchi kuhusu uhaba wa sarafu na noti za thamani ndogo kwa mahitaji ya chenji, uchakavu wa noti na kupeleka hisia za wasi wasi kuhusu ubora wanoti zilizopo kwenye mzunguuko. 

Aliwataka Wananchi kuacha kutumia noti zilizomaliza uhai wake katika mzunguuko na badala yake wazirejeshe Mabenki kwa lengo la kubadilishwa. 

Aliupongeza Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kazi kubwa unaofanya na kujituma kwao hadi kuinua hadhi ya Benki ya kwa kufikia kiwango kinachokubalika. 

Alisema kufunguliwa kwa Kituo cha Benki Kuu cha kutunzia na kuchukulia sarafu katika Benki ya Watu wa Zanzibar ni ushahidi wa wazi kuwa PBZ iko imara na kuaminiwa na Benki Kuu ya Tanzania {BOT }. 

Balozi Seif alisisitiza kwamba Kituo hicho hivi sasa kitawezesha Benki ya Watu wa Zanzibar kupunguza gharama za usafirishaji wa noti na sarafu sambamba na kuzuia uwezekano wa kupata majanga kwenye zoezi hilo. 

“ Benki imekuwa ikisafirisha wastan wa shilingi Bilioni nne hadi Tano kwa mwezi kwenda Pemba kwa miezi ya kawaida lakini usafirishaji unakuwa mara tatu kwa wiki wakati wa msimu wa Karafuu”. Alisisitiza Balozi Seif. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba Benki ya Watu wa Zanzibar itazingatia mahitaji ya wateja na kuwapatia wanachokihitaji kwa wakati hasa ikizingatiwa ishara ya kukua kwa uchumi wa Kisiwa cha Pemba uliosababishwa kufunguliwa kwa Kituo hicho. 

Akitoa Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania { BOT } Naibu Gavana wa Benki Kuu Sera za Uchumi na Fedha Dr. Natu Mwamba alisema uamuzi wa akuanzishwa kwa Vituo kama hivyo umelenga kupunguza ao kuokoa kabisa usumbufu wa upatikanaji wa Farafu hapa Nchini. 

Dr. Natu alieleza kwamba ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia Wananchi walio wengi hasa Vijijini vituo zaidi vitaongezwa katika maeneo mbali mbali Nchini. 

“ Benki Kuu ya Tanzania { BOT } tayari imeshafunguwa Vituo vya kutunzia na kusambazia noti na sarafu katika kanda za Mbeya, Mwanza, Arusha na Zanzibar na mipango iko katika hatua za mwisho kufungua chengine sumbawanga”. Alifafanua Dr Natu. 

Naibu Gavana huyo wa Benki Kuu ya Tanzania alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana lakini bado zipo baadhi ya changamoto kama baadhi ya watu kuzitumia noti wakiwa na uchafu 

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar Nd, Juma Amour Mohammed ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa kuichagua PBZ kuwa na Kituo cha kutunzia na kusambazia sarafu na noti baada ya kuridhika na vigezo vyote ilivyovitoa. 

Nd. Juma Amour alieleza kwamba uwekaji wa Kituo hicho Kisiwani Pemba ni ishara ya kukuwa kwa uchumi wa Kisiwa cha Pemba ikiwa pia miongoni mwa huduma za maendeleo kwa kusogeza huduma karibu na Jamii. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya Watu wa Zanzibar alifahamisha kwamba Benki zilizopo Zanzibar hivi sasa zitaweza kutoa huduma kwa urahisi kwa kukitumia kituo hicho.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top