Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na salama Mkoani Singida Mhandisi Issac Nyankonji  akitoa maelezo ya hatua za ujenzi wa mradi wa maji safi mkoani humo mbele ya Balozi Seif ambaye alikuwa akiangalia utekelezaji wa Serikali wa ilani ya CCM  akiwa mlezi wa Mkoa huo Kichama

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Wataalamu wa Sekta za Maji na Mazingira Nchini kuwa na utaratibu maalum utakaoiwezesha Jamii kupata elimu juu ya utunzaji wa Vianzio vya maji sambamba na utunzaji wa mazingira.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati akiukagua Ujenzi wa Mradi mkubwa wa Maji safi na salama uliopo ndani ya Manispaa ya Mji wa Singida ambao unatarajiwa kutoa huduma katika Mji huo na Vitongoji vyake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na mlezi wa Mkoa wa Singida Kichama alikuwa Mkoani humo kwa ziara ya siku mbili kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM unaofanywa na Serikali.

Alisema Serikali zote mbili zimekuwa zikiimarisha miundo mbinu ya upatikanaji wa Huduma za Maji safi Mijini na Vijijini lakini mipango hiyo wakati mwengine huonekana kupungua utekelezaji wake kutokana na uchafuzi wa vianzio vya maji na mazingira unaofanywa na baadhi ya watu kutokana na ufinyu wa Elimu na kisingizio cha ukali wa maisha.

Balozi Seif alifahamisha kwamba wataalamu hao wana kazi ya ziada katika kuhakikisha matatizo hayo yanapungua au kuondoshwa kabisa ili ile azma ya Serikali zote mbili ya Mauungano wa Tanzania na Ile ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu upatikanaji wa Maji safi inatekelezwa kupitia Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015.

“ Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010 / 2015 imezielekeza Serikali zote mbili kuendeleza program ya maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi kufikia Asilimia 65 Vijijini na asilimi 75 Mijini kwa upande wa Bara wakati asilimia 75 Mijini na asilimia 60 kwa upande wa Zanzibar ifikapo mwaka 2015”. Alifafanua Balozi Seif.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi Mkoani Singida Mhandisi Issac Nyankonji alimueleza Balozi Seif kwamba mradi huo mkubwa ulioanza ujenzi wake mwaka 2009 unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo Mwezi Aprili Mwaka huu wa 2013.

Mhandishi Nyankonji alifahamisha kwamba huduma za maji safi na salama ndani ya Mkoa wa Singida zitaondoka kabisa kwa vile mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita Milioni Tatu kwa siku kiasi ambaco kitakidhi kabisa mahitaji ya Wananchi wa eneo hilo.

Mkurugenzi huyo wa Mamlaka ya Maji safi na salama Mkoani Singida kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwanasihi na kuwaomba wananchi kuchangia huduma za Maji kwa kuwa itapatikana kwa uhakika ili mradi huo uweze kujiendesha na kurejesha imani ya wafadhili waliojitolea kusaidia kufanikisha mipango ya maendeleo Nchini.

Mradi wa Maji safi na salama Mkoani Singida umegharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni kumi na Laki Tisa { U$ 10,900,000 } sawa na Shilingi za Kitanzania Milioni thalathini na Tano { 35,000,000/- }.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuweka jiwe la Msingi la Jengo la Maabara ya Skuli ya Sekondari ya Makinya, akaweka Jiwe la Msingi la Msikiti wa Ijumaa Dung’unyi pamoja na kuweka Jiwe la msingi la Ushirika wa Saccos ya Mkinya zote zilizomo ndani ya Wilaya ya Dung’unyi.

Katika kuunga mkono juhudi za Wananchi hao Balozi Seif akiwa Mlezi wa Mkoa huo Kichama amechangia Shilingi 500,000/- kuendeleza Ushirika wa Saccos ya Mkinya , Shilingi 500,000, Vyakula na Mikoba kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Mkinya na Kuahidi kutoa mchango wa Shilingi Milioni tatu { 3,000,000/- } kusaidia uendelezaji wa ujenzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Dung’unyi.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top