Zaidi ya ekari 48 za msitu wa Hifadhi wa Jozani zimeungua moto kufuatia moto uliozuka katika msitu huo siku nne zilizopita, na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi bilioni tatu.

Akizungumza wakati akitembelea eneo hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema tukio hilo ni la kusikitisha na limeitia hasara kubwa serikali na taifa kwa ujumla.

Amesema mbali na hasara hiyo ya kiuchumi lakini moto huo pia umesababisha athari kubwa za kimazingira ambazo zinaweza kuchukua muda mrefu kuweza kurudi katika hali yake ya kawaida.

“Inawezekana baadhi ya wanyama adimu wamepotea, vyanzo vya maji vimeharibika na miti adimu ya asili imeharibika, ukweli ni hasara kubwa”, alieleza kwa masikitiko Maalim Seif.

Amewaagiza maafisa wa msitu huo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa hakuna watu wanaotumia njia za kizamani katika uvunaji wa asali ili kuepuka athari zaidi zinazoweza kujitokeza.

Maalim Seif amewataka wafugaji wa nyuki kufuata maelekezo ya wataalamu wa Wizara ya kilimo na mali asili ili kufuata njia za kisasa za uvunaji wa asali usiotumia moto ili kudhibiti uharibifu katika misitu ya asili.

“Misitu yetu ya asili tunayoitegemea zaidi ni huu wa Jozani kwa Unguja na ule wa Ngezi kwa Pemba, ni wajibu wetu tuilinde na tuihifadhi kwa nguvu zetu zote ili isitoweke”, alisisitiza Makamu wa Kwanza wa Rais.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Maliasili Dkt. Bakari Assedi amesema chanzo cha moto huo kinasadikiwa kuwa ni wavunaji wa asali wanaotumia njia za zamani za kutumia moto.

Amesema msitu huo wa asili ambao pia ni hifadhi ya taifa, ni muhimu katika kulinda na kuhifadhi misitu na viumbe adimu ambapo kwa wastani kila baada ya miaka 15 kupatikana kiumbe kipya katika msitu huo.

Amesema Wizara ya Kilimo na Maliasili imekuwa ikiwashajiisha wafugaji wa nyuki kushirikiana na Wizara hiyo kwa kupata utaalamu, na kwamba iko tayari kushirikiana nao na kuwapatia nyenzo katika jitihada za kuendeleza ufugaji wa nyuki wa kisasa.

Msitu huo pia ni muhimu kwa shughuli za kitalii ambapo watalii kutoka nchi mbali mbali hufika katika msitu huo kwa ajili ya kujionea wanyama adimu duniani wakiwemo ‘kima punju’.

Dkt. Assedi amesema moto huo unaotarajiwa kumaliza kuzimwa hii leo umeathiri zaidi miti aina ya Mikaratusi na Mitondoo.

Mapema akizungumza na wapiganaji wa kikosi cha zimamoto na uokozi katika eneo hilo, Maalim Seif amewapongeza kwa juhudi zao za kuudhibiti moto huo licha ya kukabiliwa na mazingira magumu.

Amesema serikali inathamini sana mchango wao katika harakati za kuzima moto na uokozi, na kwamba itashirikiana na kikosi hicho kwa kukipatia nyenzo zaidi ili kiweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Amewataka wapiganaji hao kuandaa mbinu zaidi za kukabiliana na maafa yoyote yanaoweza kujitokeza.

Hassan Hamad (OMKR).  

0 comments:

 
Top