Chama cha Mapinduzi kinasikitishwa na tabia inayoonekana kuanza kuchipua ya baadhi ya Wanachama wake kutumia kasoro ndogo ndogo ndani ya chama hicho kwa kususia baadhi ya masuala ya Serikali kama njia ya kutafuta ufumbuzi inaleta sura mbaya kwao na chama chao.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika mikutano tofauti wakati akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM wa baadhi ya Matawi yaliyomo ndani ya Jimbo la Kitope.

Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tabia ya baadhi ya wanachama hao kurejesha kadi kwa kisingizio cha kupatiwa ufumbuzi matatizo yao kisipotafutiwa dawa mapema kinaweza kudhoofisha nguvu za Chama hicho.

“ Wapo Wanachama walioanzisha mfumo wa kama hawakutatuliwa matatizo yao tena kwa wakati wanaoutaka wao wenyewe wanaamuwa kurejesha kadi za Chama”. Huo ni udhaifu wa Mwanachama ambao unastahiki kuachwa. Alitahadharisha Balozi Seif.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alifanya ziara hiyo kukagua baadhi ya Matawi Matano yaliyomo ndani ya Jimbo la kitope yakiwa miongoni mwa matawi 20 yaliyomo ndani ya Jimbo hilo ambayo hayajakamilika maendeleo ya ujenzi wake.

Katika ziara hiyo Balozi Seif alipata fursa ya kukabidhi baadhi ya vifaa katika Matawi ya Fujoni, Kiomba Mvua, Vuga Mkadini,Mfenesini Kwa Gube, Kitope B, na Kazole ikiwa ni pamoja na Saruji, Nondo, Matofali, mchanga, Kokoto vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 4.7.

Mapema Balozi Seif Ali Iddi akiwa Mbunge wa Jimbo la Kitope alisema hatma njema ya maisha kwa watoto wa sasa itapatikana iwapo Kamati za Maskuli,Wazazi na Walimu wataendelea kushirikiana pamoja katika kuwaandaa vilivyo Vijana wao Kitaaluma.

Alisema Vijana ndio Viongozi wa baadae wanaohitaji kufinyangwa vyema ili kuendeleza misingi bora iliyopo ya kulitumikia vizuri Taifa lao kiuzalendo na moyo thabiti.

Balozi Seif alisema hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya Skuli ya Fujoni katika mwanzo wa ziara yake ya kuangalia shughuli na miradi ya maendeleo ndani ya Jimbo la Kitope.

Mbunge huyo wa Jimbo hilo aliipongeza Kamati ya Skuli ya Fujoni, Wazee na Walimu wa skuli hiyo kwa juhudi zao kubwa zinazoleta matumaini ya kielimu kwa watoto wao.

“ Kumtengeneza Mtu asiyejua kitu akafanywa mpaka akafikia hatua ya kujua kitu ni kazi kubwa inayopaswa kupongezwa na kila muungwana”. Alifafanua Balozi Seif.

Aliishauri Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kufanya juhudi ya ziada katika kuisaidia Skuli ya Fujoni kutokana na nguvu kazi kubwa waliyoitumia ya ujenzi wa majengo yao yanayotarajiwa kutumika kwa wanafunzi wa Elimu ya Kidato cha Tano na Sita.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Maandalizi na Msingi Nd. Uledi Juma Wadi alisema Skuli ya Fujoni ni Miongoni mwa Skuli 248 za Zanzibar zilizoteuliwa kuwemo katika Mradi maalum unaotoa elimu kupitia mfumo wa Compyuta.

Nd. Uledi alisema Mradi huo { TZ 21 Century Basic Education } utakaohusisha madarasa kuanzia la kwanza hadi la nne utakwenda sambamba na skuli hizo kupatiwa computa kwa ajili ya shughuli za Kiutawala kwa Skuli hizo.

Baadae Balozi Seif akikabidhi msaada wa Vitanda Sita, magodoro,mashuka na mito yake kwa uongozi wa Kituo cha Afya cha Kiomba Mvua Vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 2,220,000/-

Akizungumza na Uongozi wafanyakazi na wananachi wanaokizunguuka Kituo hicho Balozi Seif alilaumu utaratibu mbaya wa maadhi ya wahandisi wa mamlaka ya maji wa kutoa huduma hiyo wakati wa ziara za Viongozi.

Akipokea malalamiko ya wananachi hao kutokana na tabia hiyo iliyozoeleka katika maeneo mengi Balozi Seif alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B kulifuatilia suala hilo na kumpatia maelezo dhidi ya yule ayaehusika na tabia hiyo inayoleta kero kwa wananchi. 
 
Othman Khamis Ame 
 Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top