Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijaza Fomu Maalum ya kuomba uanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar

Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Tanzania { NSSF } Umeombwa kufanya utaratibu wa kuishawishi mIfuko mengine ya Jamii kuanzisha miradi ya Jamii ili kuongeza pato la wanachama pamoja na Maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akijaza fomu maalum ya kuomba kujikunga kuwa mwanachama rasmi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } shughuli ambayo aliifanya hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema Mfuko huo umeonyesha mwanga na matumaini makubwa kwa wanachama wake hasa kutokana na miradi mingi iliyoianzisha ambayo kwa Asilimia kubwa inalenga kuwanufaisha wanachama wake hasa wale wenye kipato cha chini.

“ Kwa kweli NSSF mnastahiki pongezi za kweli kutokana na juhudi zenu mnazozitekeleza na nashangaa mfumo kama huu siuoni katika mifuko mengine. Nahisi mnawajibu wa kuisaidia kimaarifa Mifuko hii ili ifuate nyayo zenu”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alisema NSSF ni chombo cha wananchi kwa vile kinajihusisha moja kwa moja na hatma ya washirika wake ambao wengi wao ni wafanyakazi wenye kipato cha chini.

Balozi Seif aliuahidi Uongozi wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwamba amehamasika ya mfumo wa mfuko huo na kupelekea moja kwa moja kuamua kujiunga ambapo ameahidi kuchangia kila baada ya kipindi cha miezi mitatu.

Mapema Meneja wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii { NSSF } Mkoa wa Dodoma ambao ndio uliopewa jukumu la kuhudumia Viongozi wa ngazi ya Juu Bibi Maryma Ahmed alisema zaidi ya Wabunge 165 wamekubali kujiunga kwa hiari kuwa wanachama wa Mfuko huo.

Bibi Maryam alimueleza Balozi Seif kwamba wabunge hao hupatiwa mafao yao mara wamalizapo utumishi wao wa Bunge sambamba na huduma za matibabu wakati wa kipindi chote cha kazi zao.

Hata hivyo Meneja huyo wa NSSF Kanda ya Dodoma alieleza kuwa wapo Wabunge wastaafu waliomaliza wadhifa wao lakini bado wanaendelea kuchangia mfuko huo kwa vile bado wana fursa iliyo wazi ya kufanya hivyo.

Balozi Seif amesajiliwa kuwa mwanachama wa Mfuko huo wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii baada ya kukamilisha taratibu zote za kujaza fomu ya usajili mbele ya Timu ya Maafisa wa mfuko huo ikiwemo pia kupigwa picha kwa ajili ya kupatiwa kitambulisho rasmi cha uwanachama kamili wa mfuko huo.

Wakati huo huo Balozi Seif akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope amekabidhi vifaa vya ujenzi kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa Tawi la CCM la Mbaleni liliomo ndani ya Jimbo hilo.

Akikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni Mchanga, Matofali pamoja na Saruji Balozi Seif alisema wana ccm lazima waendelea kushikamana kwa lengo la kukiwezesha chama hicho kuendelea kushika dola.

Alifahamisha kwamba amani ya Tanzania itaendelea kuwepo na kuleta matumaini iwapo chama cha Mapinduzi kupitia Serikali zake zote mbili kitaendelea kuliongoza Taifa hili.

“ Wapo watu wenye mawazo ya kutaka kuipeleka Tanzania katika machafuko. Sasa Zanzibar Tanzania kwa ujumla inatarajiwa iendelee kuwa na amani. Na hii itapatikana kama CCM itendelea kuongoza”. Alisisitiza Balozi Seif.

Aliwaeleza Wananachi hao wa Kijiji cha Mbaleni kuwa anaelewa kwamba Kijiji hicho bado kina kero nyingi zinazowakabili ikiwemo bara bara na Huduma za Maji safi na salama, lakini hatua za dharura tayari zimeshachukuliwa kwa miradi miwili ya maji na bara bara ambayo inaanza kutoa matumaini.

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope aliwapongeza Wananchi hao wa Kijiji cha Mbaleni kwa ushiriki wao kwenye mchakato wa kutoa maoni kwa ajili ya kupata katioba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vifaa hivyo kwa ajili ya ujenzi wa Tawi la CCM Mbaleni Jimbo la Kitope sambamba na ahadi ya Seti moja ya Jezi na Mipira iliyotolewa na Mke wa Mbunge wa Kitope Mama Asha Suleiman Iddi vimegharimu jumla ya shuilingi Milioni Moja Nukta Tisa {1,960,000/ }.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top