Jumuiya ya Al-Yousuf imeahidi kujenga nyumba mia nne (400) za mkopo nafuu katika kijiji cha Kiuyu, Wilaya ya Micheweni Pemba.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Al-Youseif ametoa ahadi hiyo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Ofisini kwake Migombani.

Amesema mradi huo wa ujenzi wa nyumba pamoja na ule wa kilimo, inalenga kukibadilisha kijiji hicho kuwa cha kisasa na chenye maendeleo.

Amefahamisha kuwa Jumuiya yake imeshawishika kuanzisha miradi hiyo ya maendeleo, baada ya kuona kuwa wananchi wa kijiji hicho wanaishi katika mazingira magumu.

Sheikh Al-Youseif ameeleza kuwa tayari juhudi za ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi huo zimeshaanza kuchukuliwa, sambamba na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ambacho kimebainika kustawi vyema katika eneo hilo.

“Tumefanya uchunguzi tukabaini kuwa ardhi ya Kiuyu ni ya jiwe sehemu ya juu, lakini chini ni nzuri na yenye rutba, na kwamba inakubali kustawisha kilimo cha aina mbali mbali hasa cha mboga mboga”, alifafanua Sheikh Al-Youseif.

Katika hatua nyengine Sheikh Al-Youseif amekabidhi shehena ya nguo za aina mbali mbali kwa ajili ya wakaazi wa kijiji hicho cha Kiuyu Micheweni.

Nguo hizo ni pamoja na vitambaa kwa ajili ya wanawake, surauli, na shati, ikiwa na lengo la kuwasaidia wananchi hao.

Aidha ameiomba serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kumpatia orodha ya wanafunzi wote wa Kiuyu ili aweze kuwapatia sare za skuli.

Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad ameishukuru Jumuiya ya Al-Youseif kwa misaada yake kwa Zanzibar na kwamba inasaidia kupunguza tatizo la umaskini nchini.

Amesema uamuzi wa kutoa kipaumbele kwa kijiji cha Kiuyu ni sahihi, kwani ni miongoni mwa vijiji vilivyoachwa nyuma kimaendeleo kwa kipindi kirefu.

Ameeleza kuwa mradi wa kilimo ulioanzishwa katika kijiji hicho utakuwa chachu ya maendeleo, na kuwaomba wakaazi wa eneo hilo kuuenzi na kuuendeleza kwa juhudi zao zote ili uweze kuleta mafanikio.

Ameahidi kusimamia ugawaji wa nguo hizo ili kuhakikisha kuwa zinawafikia walengwa na kufikia lengo lililokusudiwa.

Hassan Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top