Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Ndugu Hassan Ali akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati alipofanya ziara fupi kuangalia harakati za wahandisi wa shirika la umeme kuondosha hitilahu iliyokikumba kituo cha kusambazia umeme mji mkongwe kiliopo Darajani
Uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar { ZECO } umeaswa kuwa makini katika taratibu zake za kutoa huduma bora kwa lengo la kupunguza kero na lawama kutoka kwa wateja wa huduma hiyo.
 
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua matengenezo ya kituo cha kusambazia Umeme katika eneo la Mji mkongwe hapo Darajani ambacho kilipata hitilafu ya umeme na kusababisha kukosekana kwa kuduma hiyo kwa karibu saa 24.

Balozi Seif alisema matumizi ya huduma za umeme hivi sasa yameongezeka mara dufu Nchini. Hivyo Shirika la Umeme iwapo halitakuwa makini katika kukabiliana na ongezeko hilo lawama zaidi zitaendelea kulipata shirika hilo.

Aliuagiza uongozi wa Shirika hilo kupitia Waziri wake kufanya utaratibu wa kuyawasilisha yale matatizo ambayo hayamo katika uwezo wao na serikali kwa upande wake itajaribu kutafuta mbinu ya muyatatua.

“ Uongozi wa Shirika lazima uelewe kwamba matumizi makubwa ya huduma za umeme yameongezeka zaidi kiasi ambacho kinaonekana kuleta chngamoto kwa shirika hilo”. Alifafanua Balozi Seif.

Aliwaagiza wahandisi wa shirika hilo kufanya kazi ya ziada hasa wakati wa kukabiliana na hitilafu za umeme zinapojitokeza katika sehemu mbali mbali hapa Nchini.

Mapema Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar Nd. Hassan Ali alimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba wahandisi wa shirika hilo wamelazimika kuongeza mtandao wa Umeme katika eneo hilo ili kupunguza hitilafu inayojitokea kila mara katika kituo hicho.

Ndugu Hassan alifahamisha kwamba mtandao uliopo hivi sasa ndani ya eneo lote la mji Mkongwewa Zanzibar tayari umeshaonyesha dalili ya kuzidiwa na wateja kutokana na kukua kwa matumizi ya huduma hiyo muhimu.

Kituo cha kusambazia huduma ya umeme ndani ya Mji Mkongwe kiliopo Darajani Mjini Zanzibar kimekuwa kikikabiliwa na hitilafu ya mara kwa mara ya umeme la kusababisha usumbufu wa kukatika katia kwa umeme katika eneo hilo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika Mtaa wa Bububu Kijichi kumpa pole Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Juma Ali kufuatia nyumba yake kuungua moto.

Ajali ya moto huo iliyosababishwa na hitilafu za umeme imetokea mapema asubuhi na kuathiri chumba cha watolto pamoja na baadhi ya seheme za dari ya nyumba hiyo.

Akielezea mkasa huo Ndugu Juma alimeleza Balozi Seif kwamba juhudi za majirani na baadae kikosi cha zima moto na uokozi ndizo zilizosababisha kuudhibiti moto huo.

“ Kwa kweli sina cha kusema wala cha kuwalipa majirani zangu kutokana na uungwana waliouonyesha ambao sijapa kuushuhudia katika maisha yangu. Nilishangaa hata simu na Mama Watoto wangu iliyokuwa imeokolewa katika kizaa zaa hicho nililetewa, tabia ambayo ni nadra katika baadhi ya mitaa tuliyokuwa tukiishi”. Alielezea faraja yake Ndugu Juma.

Akimfariji Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Nd. Juma Ali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliikumbusha Jamii kupenda utamaduni wa kuweka Bima mali zao ili kuwasaidia wakati wanapopatwa na Majanga na hatimae Maafa.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top