Mkurugenzi Mkuu wa Tasaf Tanzania Bwana ladislausd Mwamanga akitoa ufafanuzi wa Hataua za Tasaf katika Awamu ya Tatu ya Miradi yake mbele ya  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania { Tasaf } Bwana Ladislaus Mwamanga alisema Mradi wa Tasaf Awamu ya Tatu unatarajiwa kulenga zaidi katika miradi ya Elimu, Afya na Maji safi ili kusaidia zaidi kupunguza umaskini kwa wananchi wenye mazingira magumu.

Hatua hiyo itakwenda sambamba na uimarishaji wa Uongozi katika mifumo ya utekelezaji wa miradi hiyo ya Tasaf awamu ya Tatu ambayo ni muhimu kwa maslahi ya wananchi walio wengi.

Bwana Ladislaus Mwamanga alieleza hayo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi watano wa Tasaf kutoka Makao Makuu Mjini Dar es salaam wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Alieleza kwamba Tasaf awamu ya tatu imekusudia kupanua wigo kwa kuendelea kuzishirikisha Halmashauri za Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara wakati Zanzibar zitaendelea na hatua ya awali kwa shehia 20 kwa kuzijengea mifumo ya utekelezaji.

Mkurugenzi huyo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania alisema Zanzibar imefanikiwa vyema katika utekelezaji wa Tasaf awamu mbili zilizopita na kuiomba Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambayo ndio inayoratibu shughuli za Tasaf Zanzibar kumteuwa Ofisa atakayekuwa na majukumu ya Kuratibu shughuli zote za Tasaf kwa upande wa Zanzibar.

“ Tumefarajika sana kuona mipango tuliyoipanga katika utekelezaji wa Tasaf awamu ya Pili Zanzibar imefanikisha vya kutosha lakini kumekuwa na hitilafu ya utekelezaji katiba baadhi ya Halmashuri kwa upande wa Tanzania Bara”. Alifafanua Bw. Ladislaus Mwamanga.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisisitiza suala la kuongezwa Taaluma kwa watendaji wanaosimamia Miradi ya Tasaf katika maeneo mbali mbali Nchini.

Balozi Seif alisema kumekuwa na ubadhirifu na matumizi mabovu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya wasimamizi wa miradi hiyo katika awamu zilizopita tabia ambayo imezorotesha kutokukamilika au kufa kabisa kwa baadhi ya miradi hiyo.

Aliwaasa watendaji wote wanaopewa jukumu la kusimamia miradi ya Tasaf kujitahidi kuzingatia uadilifu ili kuepuka ujanja unaobuniwa na baadhi ya mahujumu wa miradi hiyo kwa maslahi binafsi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Tasaf kwa uamuzi wake wa kuzingatia zaidi kutoa Taaluma kwa watendaji watakaopewa jukumu la kusimamia miradi ya Tasaf.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kutoa msukumo ili kuona Miradi ya Tasaf inatekelezwa vyema kwa vile imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Zanzibar katika kuelekea kwenye maendeleo. 


Othman Khamis Ame  
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


0 comments:

 
Top