Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa eneo la Kihistoria Kati ya Muekezaji na Wanakijiji wa Bweleo ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi akimkabidhi rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Baliozi Seif Ali Iddi ripoti ya uchunguzi wa mgogoro huo  na mapendekezo yanayostahiki kuchukuliwa 
Mwenyekiti wa Kamati Maalum iliyoundwa kuchunguza mgogoro wa eneo la Kihistoria Kati ya Muekezaji na Wanakijiji wa Bweleo ambae ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi amekabidhi rasmi ripoti ya uchunguzi huo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Baliozi Seif Ali Iddi.

Eneo hilo la Ekari Tatu lenye magofu ya Kihistoria limekuwa likilalamikiwa na Wananachi hao dhidi ya muwekezji aliyepewa eneo hilo Bwana Chandra wakidai kwamba ameshindwa kuliendeleza kiuwekezaji kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Makabidhiano hayo yaliyoshuhudiwa pia na wajumbe wa Kamati hiyo iliyojumuisha wataalamu wa mazingira, Utalii, Uwekezaji, Wanasheria pamoja na Wawakilishi wa wana Kijiji yamefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar iliyopo Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Akitoa muhtasari wa Ripoti yenyewe Katibu wa Kamati hiyo ambae pia ni Afisa Tawala wa Mkoa Mjini Magharibi Nd. Ayoub Mohammed Mahmoud alisema ripoti hiyo iimebeba mapendekezo tisa yaliyofanyiwa uchambuzi wa kitaalam.

Nd. Ayoub alisema Kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yake ililazimika kuwahoji Wananchi 40 , Muwekezaji,Taasisi Sita zinazojihusisha na masuala ya uwekezaji, mazingira na Utalii sambamba na kupitia kumbu kumbu za makubaliano kati ya muekezaji huyo na Wananchi.

Katibu wa Kamati hiyo alifahamisha kwamba miongoni mwa Mapendekezo hayo Tisa kubwa zaidi ni la kuishauri Serikali kuiangalia upya sheria ya Mikataba ambayo wamelenga kuwa baina ya Serikali yenyewe na Muwekezaji ili kuepuka mikataba zaidi ya mmoja ambayo ndio chanzo cha migogoro inayojitokeza.

Aliyataja baadhi ya Mapendekezo hayo kuwa ni umuhimu wa utunzwaji wa Kumbukumbu za Taasisi za Serikali, kuangaliwa kwanza kwa maslahi ya Kijamii pamoja Serikali kutoa Taaluma maalum kwa wananachi juu ya suala la ushirikiano wao na wawekezaji.

Akitoa shukrani zake kwa kazi kubwa iliyotekelezwa na Kamati hiyo Maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali imeamua kuteua Kamati hiyo ili kuondosha joto lililochomoza kati ya pande hizo mbili zinazohitilafiana.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaipitia vyema ripoti hiyo na hatiame kutoa maamuzi yatakayozingatia sheria na taratibu zilizopo ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo bila ya kuonea upande wowote.

“ Nia ya Serikali wakati wote si kuwadhalilisha wawekezaji bali kinachohitajika na kuzingatiwa zaidi wakati wote ni kufuatwa kwa Sheria na Taratibu zilizopo hapa Nchini ”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Mwenyekiti wa Kamati hiyo Maalum ya mgogoro wa eneo la Kihistoria baina ya Wananchi wa Kijiji cha Bweleo na Muwekezaji, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Abdulla Mwinyi alisema Wajumbe wa Kamati hiyo wako tayari wakati wote kutekeleza agizo lolote la Serikali kwa maslahi ya Taifa.

Mh. Abdulla Mwinyi alimueleza Balozi Seif kwamba ripoti hiyo iliyoandikwa kitaalamu inaweza kufanywa hadidu rejea kwa migogoro mengine inayofanana na ule wa Bweleo kwa kuwa imehusisha washirika karibu sekta zote zinazohusika na masuala ya uwekezaji Vitega Uchumi.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top