Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kufanya juhudi  za ziada katika kukiimarisha kitengo cha  Viungo na Vilema Kiliopo katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ili kiwe na uwezo wa kuhudumia wagonjwa kwa ufanisi zaidi.
Ombi hilo limetolewa na Wafanyakazi wa Kitengo hicho chini ya Usimamizi wa Mkuu wake Dr. Adam Haji Makame wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua  shughuli za kazi za Kitengo hicho.
Wafanyakazi hao walimueleza Balozi Seif kwamba Kitengo hicho kimekuwa kikitoa huduma kwa kutumia vifaa vya zamani pamoja na Wafanyakazi hafifu kulingana na idadi kubwa ya Wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Walisema ipo haja kwa Serikali Kuu kufanya utaratibu wa haraka wa kuwasomesha   Vijana  waliomakini ambao watakuwa na moyo na uzalendo wa kusaidia Jamii yao.
“ Tumekuwa tukishuhudia Vijana wengi wanaosomea kada hii lakini cha kushangaza wamalizapo tuu mafunzo yao hata yale ya cheti huingia Mitini jambao ambalo linatuiwa vigumu sisi tunaohitaji kusaidia kazi hii”.  Walisema wafanyakazi hao wa Kitengo cha  Viungo na Vilema.
Walifahamisha kwamba Kitengo hicho kimekuwa kikipokea wagonjwa zaidi ya 1300 kwa mwezi wanaohitaji huduma za hapo lakini uwezo wa kuhudumia wagonjwa hao ni mdogo hasa ikizingatiwa uhaba wa Vifaa na Wafanyakazi.
Hata hivyo wafanyakazi hao pia wanalazimika wakati mwengine kuandaa   ratiba ya kuwafuata wagonjwa wengine katika maeneo ya   hapa Zanzibar kulingana na hali ya ulemavu wa baadhi ya wagonjwa  ambao wako Vijijini.
Akitoa shukrani zake kwa Wafanyakazi  hao wa kitengo cha Viungo na Vilema kutokana na kazi kubwa inayowakabili kila siku Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali itaangalia uwezekano wa kufanya mageuzi katika kitengo hicho.
 Balozi Seif alifahamisha kwamba hatua hiyo inaweza kukifanya Kitengo hicho kufanya kazi zake kwa ufanisi na kitaalamu zaidi.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alilikaguwa Jengo la  itakayokuwa        Ofisi Kuu ya Bodi ya Chakula ,Dawa na Vipodozi liliopo Mtaa wa Mombasa.
Jengo hilo lililokuwa la Kiwanda cha Kampuni ya Uchapaji wa Al- Khayria linahitaji kufanyiwa matengenezo makubwa kufuatia baadhi ya Vifaa vyake likiwemo paa kuibiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar Nd. Burhan Othman Said alisema  kazi iliyopo hivi sasa ni kulifanyia matengenezo makubwa Jengo hilo licha ya uchafuzi wa mazingira kwa kuchimbwa mchanga unaofanywa na baadhi ya watu pembezoni mwa jengo hilo.
Akizungumza na Uongozi huo Balozi Seif ameiagiza Wizara ya Afya kufanya utaratibu wa kuliezeka kwa haraka jengo hilo ili kujaribu kusaidia  kukabiliana na hali hiyo.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwapongeza  Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na Wananchi wa Kijiji cha Bweleo kwa ari yao kubwa ya kujiletea Maendeleo.
Balozi Seif alitoa pongezi hizo mara baada ya Sala ya Ijumaa Katika Msikiti wa Kijiji hicho alipokuwa akisalimiana na Waumini hao wa Dini ya Kiislamu.
Alisema utaratibu wa Wananchi hao wa kujitatulia kero na matatizo yanayowakabili ni kitu kizuri kwani huleta faraja shauku ya kusaidia na wapenda maeneleo popote pale.
“Huu ni miongoni mwa Misikiti michache hapa Nchini ambayo imejengwa na Waumini wenyewe bila ya kutegemea nguvu za wafadhili”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi na Waumini hao kwamba  ataangalia utaratibu wa kusaidia ujenzi wa vyoo na sehemu ya  kutawadhia katika Msikiti huo wa ijumaa.
Othman Khamis Ame   
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar            

0 comments:

 
Top