Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inatarajia kupokea Msaada wa Mashine za Uchunguzi wa Damu { DNA } wakati wowote
kuanzia Mwezi wa Julai Mwaka huu kutoka Taasisi inayoshughulikia Taaluma ya Teknolojia
ya Afya ya Chuo Kikuu cha Brown Mjini Boston
Nchini Marekani { MED International }.
Msaada huo unafuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya Mwezi wa Oktoba Mwaka uliopita
Nchini Marekani ambapo alipata fursa ya kufanya kwa mazungumzo na Uongozi wa juu wa Taasisi
hiyo.
Mwakilishi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya
MED International Bwana Jayson Marwaha alieleza hayo wakati alipofanya
mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Jayson akiwa na Mkurugenzi mwenza wa Taasisi
hiyo Bwana Han Sheng Chia amemueleza
Balozi Seif kwamba sambamba na Msaada huo wamekuja Zanzibar
kufanya Utafiti wa Afya katika Hospitali tofauti za Serikali za Unguja na Pemba.
“ Lengo letu la kufanya Utafiti huo hapa Zanzibar ni kuangalia
maeneo na vifaa gani vinahitajika na tutakaporejea kwenye Taasisi yetu tuweze
kuyachukulia hatua kwa nia ya kuimarisha Ustawi wa Jamii hasa ile ya kawaida”.
Alifafanua Mkurugenzi huyo wa MED International.
Bwana Jayson alieleza kwamba katika kuona Taaluma ya
kiuhandisi ndani ya Sekta ya Afya inakuwa Kiteknolojia Taasisi yake inatarajia pia kuleta Mabingwa wa fani hiyo
mnamo Mwezi wa Agosti Mwaka huu.
Katika Mazungumzo yao Nchini Marekani Mwaka jana Bwana Jayson aliwahi kumuahidi Balozi Seif
kwamba Taasisi yake itaandaa taratibu kwa
Wataalamu wake kufanya kazi za kujitolea Hapa Zanzibar.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Taasisi hiyo inayoshughulikia
Taaluma ya Teknolojia ya Afya { MED International kwa uamuzi wake wa kusaidia
huduma za Afya hapa Zanzibar.
Balozi Seif ameelezea kufarajika kwake na ujio wa
Uongozi wa juu wa Taasisi hiyo ambao umeonyesha uungwana katika kutimiza ahadi
zake ilizozitowa Mwaka jana Nchini Marekani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliueleza Ujumbe huo wa Med
International kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuimarisha zaidi
huduma za Afya katika Hospitali zake zote Unguja na Pemba.
Mapema Naibu waziri wa Afya Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya
alisema Ujumbe huo umekuja wakati muwafaka kwa vite bado eneo la Fani ya Sayansi
katika chuo cha Sayansi ya Afya Mbweni linahitajika.
Ujumbe huo wa MED International tayari umeanza
kukutana na washirika wao wa Sekta ya Afya hapa Zanzibar katika kujiandaa na Taratibu za
kuanza Utafiti huo unaotarajiwa kuendelea hadi Septemba 2 Mwaka huu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi amekabidhi msaada wa gari moja kwa ajili ya matumizi ya shughuli za
Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz ya Fuoni.
Balozi Seif alisema ameamua yeye binafsi kupitia wafadhili
pamoja na Familia yake kutoa msaada huo kutokana na mchango mkubwa unaotolewa
na Jumuiya hiyo ndani katika kueneza Daawa kwa Jamii.
Balozi Seif ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kutojiingiza
katika masuala ya Kisiasa na kuahidi kutoa mchango wa Shilingi 500,000/-
kusaidia harakati za Taasisi hiyo.
Mapema katibu wa Jumuiya ya Fiy Sabilillah Markaz ya
Fuoni Sheikh Mwalimu Hafidh Jabu ameuomba Uongozi wa Serikali kuwa karibu zaidi
na Jumuiya hiyo kwa lengo la kufanikisha majukumu waliyojipangia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Ali
Khamis amesema kitendo cha Serikali Kupitia Wizara ya Miundo Mbinu na
Mawasiliano kuifanyia matengenezo Bara bara ya Fuoni hadi Markaz kinafaa
kupongezwa na kushukuriwa.
Sheikh Ali alisema bara bara hiyo hivi sasa imeleta
faraja kwao na hata kwa Wananchi wa Eneo la Fuoni ambao kwa kipindi kirefu
walikuwa wakikabiliwa na Tatizo sugu la ubovu wa Bara bara hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment