Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Taasisi inayojihusisha na Masuala ya Gas { RAK GAS } ya Nchini Ras Al Khaimah Bwana Kamal Ataya aliyeuongoza Ujumbe wa Viongozi watano wa Taasisi hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Kamal na ujumbe wake wako Zanzibar kufuatia mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wakati wa ziara yake Nchini Ras Al Khaimah hivi karibuni .
Alisema lengo la mazungumzo hayo ya kujenga uhusiano ni kufanya kazi pamoja katika kuona Maendeleo ya Mataifa hayo Mawili yanakuwa Kiuchumi.
Bwana Kamali Ataya alifahamisha kwamba Taasisi yao imejikita zaidi katika uimarishaji wa Sekta za Uchumi, Kilimo, Uvuvi, Elimu na Hata Sekta ya Afya.
“ Tumejipanga vyema na tuko tayari pia kutoa Mafunzo katika Sekta ya Mafuta hasa zaidi katika fani ya ufundi”. Alisisitiza Bwana Kamal Ataya.
Kiongozi huyo wa Taasisi ya RAK Gas alimueleza Balozi Seif kwamba dalili za matumaini zimeanza kujichomoza kufuatia Mazungumzo yao ya mwanzo na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa sekta tofauti hapa Zanzibar .
Aidha Bwana Kamal alieleza kuwa taasisi yake itahakikisha kwamba yale maeneo yatakayofikia hatua za makubaliano ya pande hizo mbili yanaanza kuchukuliwa hatua mara moja.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliupongeza Ujumbe wa Taasisi hiyo kwa hatua zake ilizochukuwa za kufuatilia makubaliano ya pande hizo mbili katika kipindi kifupi.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe wa huo kwamba Taifa lina matumaini makubwa ya kunyanyuka zaidi kwa Uchumi wake kutokana na muelekeo wa Taasisi hiyo kuelekeza nguvu zake hapa Zanzibar .
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali imekusudia kuelekeza nguvu zake katika kuwapatia elimu zaidi Vijana katika nyanja ya Utalii kwa lengo la kujijengea uwezo wa ajira katika Sekta hiyo ambayo imekuwa muhimili mkubwa wa Uchumi.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na Hoteli nyingi za Kitalii za Daraja la juu lakini idadi kubwa ya wafanyakazi wake inaonekana kutoka nje ya Zanzibar .
“ Zipo Hoteli nyingi za Kitalii ambazo zimetoa ajira kadhaa hapa Zanzibar lakini kinachoonekana Vijana wengi wanakosa kuajiriwa kutokana na ukosefu wa taaluma ya fani hiyo”. Alifafanua Balozi Seif.
Ujumbe wa Taasisi hiyo ya Masuala ya Gas { RAK GAS } ya Ras Al Khaimah umekuja kuangalia maeneo yepi ya mwanzo yanaweza kuchukuliwa hatua za utekelezaji wa makubaliano ya pande hizo mbili katika kuimarisha Uchumi wa Nchi hizo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment