Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anaondoka Nchini leo kuelekea Nchini Cuba Kupitia Nchini Israel kwa ziara ya wiki mbili ya Kiserikali.
Balozi Seif katika ziara hiyo anafuatana na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mh. Mohammed Aboud Mohammed na Mkurugenzi wa Idara ya Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad kwa upande wa Israel wakati ziara ya Cuba ataambatana na Waziri wa Afya Mh. Juma Duni Haji pamoja na Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dr. Malik Abdulla Juma. Akipitia Nchini Israel Balozi Seif anatarajiwa kukutana na Uongozi wa Taasisi zinazosimamia na kushughulikia masuala ya Maafa, Uokozi pamoja na majanga ya Matetemeko.
Hatua ya ziara hiyo imelenga kuimarisha juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha kwamba inakuwa na uwezo zaidi wa kukabiliana na Maafa na Majanga kwa haraka wakati yanapotokea.
Akiwa Nchini Cuba Balozi Seif na Ujumbe wake anatarajiwa kukutana na Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Nchi hiyo katika suala zima la Kuimarisha Uhusiano uliopo wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
Uhusiano huo utalenga zaidi katika masuala makubwa ya Sekta ya Afya ambapo Cuba imekuwa mshirika mkubwa wa Zanzibar katika kusaidia huduma za Afya katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita.
Zanzibar hivi sasa inaendelea kufaidika na huduma za Madaktari Bingwa wa Cuba wanaoendelea kutoa huduma za Afya pamoja na Mafunzo kwa Madaktari 50 Wazalendo wanaotarajiwa kuhudumia Hospitali mbali mbali za Unguja na Pemba mara baada ya kumaliza mafunzo yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi atamaliza ziara yake Tarehe 19 Mei na kupitia Rasil Heyma kwa mualiko wa Mfalme wa Nchi hiyo Bwana Saoud Bin Qasimi.
Viongozi hao wawili watapata fursa ya kuzungumzia Miradi kadhaa ya Nchi hiyo inayokusudiwa kuwekezwa hapa Zanzibar ikiwa na lengo la kuimarisha uhusiano wa pande hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kurejea nyumbani Tarehe 22 Mei mwaka huu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top