UJUMBE WA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA KUONGEZA UELEWA WA MARADHI YA usonji  ULIMWENGUNI, 2 Aprili 2012 Usonji(autism) haupo katika eneo au nchi moja tu, bali ni changamoto kwa ulimwengu, inayohitaji kushughulikiwa na dunia nzima.
Licha ya kuwa hali ya kudumaa na kutojiweza kama maradhi ya usonji yalivyo huanza utotoni, hudumu katika kipindi chote cha maisha ya mtu. Kazi yetu ya pamoja kwa ajili ya watu wenye maradhi haya isiishie tu katika kuung’amua mapema au kutoa matibabu, shurti ijumuishe uponyaji, mipango ya kielimu na hatua nyingine endelevu zitakazodumu katika kipindi chote cha maisha.
Kuwafikia watu wenye namna mbalimbali za maradhi ya usonji kunahitaji dhamira ya dhati ya  kisiasa ya ulimwengu mzima, pia ushirikiano bora wa kimataifa, hasa katika kushirikishana uzoefu. Uwekezaji mkubwa zaidi kwenye sekta za jamii, elimu na kazi ni muhimu kabisa, kwani nchi zilizoeendelea na zinazoendelea sawia zinahitaji kujiongezea uwezo wa kushughulikia mahitaji muhimu ya watu wenye usonji na kuimarisha vipaji vyao. Twahitaji kuhamasisha utafiti zaidi, kutoa mafunzo kwa watunza wagonjwa wasio na utaalamu maalum, na kuiwezesha jumuiya ya wenye usonji kuifikia mifumo ya matunzo ili kupata huduma zitakazowasaidia na kujenga mtandao wa watu wenye usonji.
Maadhimisho ya kila mwaka ya Siku ya Usonji Ulimwenguni yanakusudia kuchochea na kumulika ubaguzi usiokubalika, unyanyasaji na utengaji wa watu wenye usonji na wapendwa wao. Kama ilivyosisitizwa na Azimio la Haki za Watu wenye Ulemavu, waathirika wa usonji ni raia sawasawa na wengine, tena wanatakiwa wanufaike na haki zote za binadamu na uhuru wa mwanadamu.
Katika siku hii ya leo hapa New York, Vienna na Geneva, Shirika la Posta la Umoja wa Mataifa linazindua stempu sita za kumbukumbu na aina mbili za bahasha zitakazotolewa kwa ajili ya kuhamasisha uelewa wa maradhi ya usonji. Vipande hivi vidogo vya karatasi—vikiwa na picha zilizobuniwa na wachoraji waliogunduliwa kuwa na maradhi ya usonji—vitapeleka ujumbe wenye nguvu kwa watu duniani kote, kwamba vipaji na ubunivu vi hai ndani yetu sote.   
Mke wangu amekuwa akijishughulisha sana na uenezaji wa uelewa wa ugonjwa wa usonji. Mke wangu amenisimulia habari kuhusiana si tu za watu wenye usonji, bali pia wale waliojitoa kuboresha maisha ya waathirika hao. Tuendelee kushirikiana bega kwa bega ili kuwawezesha wenye maradhi ya usonji au dosari nyingine za akili watambue uwezo wao, hivyo wafurahie fursa na ubukheri ambavyo ni haki yao ya kuzaliwa.

0 comments:

 
Top