Kasi ya Maendeleo ya Wananchi katika sekta ya Elimu kwenye maeneo mbali mbali Unguja na Pemba inaonekana kupamba moto katika dhana nzima ya kuwajengea mazingira bora ya kielimu watoto wao.
Mkurugenzi Uendeshaji, Sera na Mipango wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bibi Madina Mwinyi Mjaka alitoa kauli hiyo katika hafla fupi ya kukabidhiwa Mabati 114 kati ya 154 kwa Skuli ya Upenja yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.
Bibi Madina alisema Bajeti ya Wizara ya Elimu ya Mwaka 2011/2012 ni kukamilisha uwezekaji wa majengo ya Skuli 500 Zanzibar nzima na hadi sasa ni Majengo 200 tu yaliyokamilika uwezekaji wake.
Alisema licha ya uwezo mdogo wa Wizara ya Elimu wa kukamilisha majengo hayo kulingana na kasi kubwa ya Wananchi katika ujenzi wa Majengo tofauti Wizara hiyo imelazimika kuyakamilisha majengo ya skuli ya Upenja nje ya Bajeti yake kutokana na Msaada mkubwa uliotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kitope.
Mkurugenzi Madina alimpongeza Balozi Seif kwa jitihada zake za kuiunga mkono Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuchangia baadhi ya harakati za uwezekaji licha ya kwamba kazi hiyo ni jukumu la Wizara ya Elimu.
“ Tunafaa kumfyagilia Balozi Seif kwa kuunga Mkono Wizara yetu, lakini pia ni Taifa zima. Tungekuwa na Viongozi kama hawa katika maeneo yetu bila shaka Zanzibar ingekuwa mbele sana Kimaendeleo zaidi ya ilipo hivi sasa”. Alifafanua Mkurugenzi Madina.
Akikabidhi Mabati hayo 114 kwa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Upenja Ndugu Juma Saleh Abass Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi aliwakumbusha Wazazi kuendelea kuwajengea mazingira mazuri ya Kielimu Watoto wao.
Alisema tabia ya tamaa ya fedha inayoendelea kufanywa na baadhi ya Wazazi kwa kuwaozesha watoto wao mapema ni kuwadumaza kimaisha jambo ambao litaongeza mzigo wa matatizo ndani ya Familia.Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alikabidhi mabati 67 na kuahidi kutoa mchango wa Shilingi 500,000/- kwa ajili ya shughuli za uwezekaji wa Maskani ya Wazee ya Tungalipo iliyopo Pwani Mchangani.
Mabati hayo ni ahadi aliyoitowa ndani ya kipindi cha siku 28 kufuatia ziara yake kwenye Maskani hiyo mwezi Machi mwaka huu.
Balozi Seif pia akakabidhi milango 10 na Madirisha Manane kwa Mwenyekiti Mzee Mikidadi Adam wa Tawi la CCM Kitope A ambalo ni Tawi Mama ndani ya Jimbo la Kitope lililozaa Matawi sita hadi sasa.
Baadaye Balozi Seif Alikabidhi Mabati 65, Milango na Madirisha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi na uwezekaji wa Tawi la CCM la Matetema Kazole.
Jumla ya Shilingi Milioni kumi na nane na Laki tisa {18,900,000} zimetumika kusaidia kugharamia Miradi hiyo ya Jamii na ile ya Chama cha Mapinduzi.
Akizungumza katika Mikutano tofauti Balozi Seif alisema nia ya chama cha Mapinduzi ni kuona Ofisi zake zilazojengwa kuanzia Matawi hadi Mikoa zinalingana na hadhi ya Chama chenyewe.
Alisisitiza kwamba wakati umefika kwa Wana CCM hivi sasa kuendelea kufanya kazi zao ndani ya Ofisi badala ya ile tabia ya baadhi ya Matawi hayo kutekeleza majukumu yao Chini ya Miembe.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kuitembelea Madrasa ya Nuuru llah iliyopo katika Kijiji cha Kitope ndani kuona maendeleo ya Elimu ya Watoto wa Madrasa hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top