Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itakuwa tayari wakati wote kupokea mawazo yatakayotolewa na Wataalamu wa Mpango wa Nchi za Kiafrika kujitathmini Kiutawala Bora katika dhana nzima ya kutandika Demokrasia ndani ya Visiwa vya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo wakati wa Mazungumzo yake na Ujumbe wa Mpango huo uliopo Zanzibar kwa ziara maalum ya Kutathmini Utawala Bora.
Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo wa APRM unaoongozwa na Rais wa Taasisi ya Utawala Bora Nchini Cameroun Bwana Barrister Akero Muna kwamba licha ya Zanzibar kuwa na utulivu wa Kisiasa lakini bado inahitaji kupata Mawazo zaidi ya Wataalamu katika kuelekea kwenye Demokrasia makini.
Alisema Zanzibar inalazimika kuwa na utulivu mkubwa miongoni mwa Wananchi wake kutokana na historia ndefu ya migogoro ya Kisiasa iliyopelekea kuduma Maendeleo ya Jamii.
“ Tumeshuhudia mivutano mikubwa ya kisiasa ndani ya Zanzibar tokea katika miaka ya 50 hadi miaka ya 2000 iliyozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Wananchi wake kuchoshwa na kadhia hiyo”. Alifafanua Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali hivi sasa inaangalia zaidi matakwa ya Wananchi katika misingi ya kuwaletea Maendeleo makubwa.
Naye Kiongozi wa Ujumbe huo wa APRM Bwana Barrister Akero Muna alimueleza Balozi Seif kwamba Ujumbwe wao upo Zanzibar kufuatilia Ripoti yao ya Utawala Bora kwa Upande wa Zanzibar.
Bwana Muna alisema Ziara yao inahusisha kukutana na Viongozi wa Serikali, Taasisi za Serikali na zile Binafsi zilikemo pia Jumuiya za Kiraia.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa pia Mbunge wa Jimbo la Kitope alipokea Mchango shilingi Milioni moja kutoka kwa Mh. Haroun Ali Suleiman .
Mchango huo ameutoa Waziri Haroun kufuatia ahadi yake aliyoitoa kwenye sherehe za Jimbo la kitope mwaka uliopita hapo Skuli ya Mgambo wakati alipokuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
Mh. Haroun ambae kwa sasa ni Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika alisema ameguswa na Maendeleo ya Jimbo hilo yaliyosababishwa na ukaribu wa Wananchi na Viongozi wao.
Waziri Haroun alielezea furaha yake kutokana na kasi kubwa ya Ujenzi wa Majengo Mapya ya Skuli yakiwemo yale ya ghorofa ambayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia matumizi mazuri ya ardhi ndogo.
Akipokea Mchango huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alimpongeza Waziri Haroun kwa ukereketwa wake wa Maendeleo ya Wananchi hasa zaidi katika Sekta ya Elimu.
Balozi Seif alisema Hamasa za Waziri Haroun zimechangia ongezeko kubwa la Ujenzi wa Skuli tofauti Nchini na matokeo yake inaendelea kuleta matunda.
Othmana Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top