Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na Masuala ya Miundo Mbinu kutoka Nchini India inaendelea na utaratibu wa kuangalia Mipango yao zaidi katika kuongeza nguvu za Uwekezaji Barani Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Ujumbe wa Viongozi wa juu wa Kampuni hiyo ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Hapo Ofisi ya Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Balozi Vidya Bhushan Soni alimueleza Balozi Seif kwamba zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 5.4 zimetengwa katika Bajeti ijayo kwa ajili ya kushughulikia Miradi mbali mbali Barani Afrika.
Alisema Kampuni hiyo tayari imeshawekeza kwenye miradi ya Umeme na uzalishaji wa Sukari katika Nchi za Ethiopia na Msumbiji lengo likiwa ni kusaidia msukumo wa Maendeleo barani Afrika.
“ Mtazamo wetu hivi sasa ni kuelekeza nguvu zaidi katika Mataifa ya Sudan Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Tanzania na baadaye Kenya na Uganda”. Alisisitiza Balozi Vidya.
Balozi Vidya alieleza kwamba Taasisi yake inaangalia utaratibu wa kuunga mkono jitihada za Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } katika mpango wa usambazaji maji kwa Wananchi.
Halkadhalika Balozi Vidya alimueleza Balozi Seif kwamba mkazo zaidi utawekwa katika Miradi ya Mawasiliano, Maji, Umeme pamoja na Uzalishaji wa Sukari.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe wa Kampuni hiyo ya Kimataifa ya Miundo Mbinu Nchini India kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga katika uimarishaji wa Viwanda vidogo vidogo vya matunda.
Balozi Seif alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na Matunda mengi lakini kinachokosekana ni ukosefu wa Utaalamu pamoja na Viwanda katika usindikizaji wa mazao hayo.
Aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo kuliangalia pia eneo hilo ambalo ni muhimu hapo baadaye kwa kutoa ajira kwa vile soko la mazao hayo linapatikana zaidi Mashariki ya Kati.
“ Mtazamo uliopo ni kuwa na Viwanda vitakavyokidhi usindikaji ulio bora wa mazao hayo ili kufikia kiwango kinachokubalika Kimataifa”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akigusia Sekta ya Utalii Balozi Seif aliufahamisha Ujumbe huo kwamba bado una nafasi ya kuangalia namna unavyoweza kuwekeza katika Biashara ya Utalii hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali hivi sasa imeongeza nguvu zake katika kuimarisha miundo mbinu kwenye Sekta ya Utalii kwa lengo la kuvutuia Wawekezaji zaidi.
Alisema Sekta hiyo hivi sasa imepewa msukumo mkubwa kwa vile inaweza kusaidiana na zao la Karafuu katika kuliongezea mapato zaidi Taifa.
Mwenyekiti huyo wa kampuni ya Kimataifa ya Miundo mbinu Nchini India Balozi Vidya Bhushan Soni aktika ziara hiyo pia ameambatana na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bwanan AustineSequeira, Mkurugenzi Masoko na Biashara Bw.Chandersekhar Gupta na Mkuu wa Mauzo AnupanGupta.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top