Jamuhuri ya Watu wa China itaendelea kuwa Mshirika mkubwa wa Zanzibar katika harakati za Uimarishaji wa Maendeleo ya Kiuchumi Kibiashara, Miundombinu na Ustawi wa jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Ujumbe wa Kampuni ya Ujenzi wa Reli Nchini China {CRCG} ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo Bwana Liu Rongyao.
Balozi Seif alisema jamii imeshuhudia juhudi za China zinavyozidi kuongezeka katika kuona Zanzibar inajikwamua katika wimbi la umasikini kupitia kasi za uimarishaji miundo mbinu. Aliyapongeza Makampuni mbali mbali ya China yanayotowa huduma zake hapa Zanzibar hasa yale ya Ujenzi ambayo kwa kiasi kikubwa yanaendelea kuchangia mabadiliko ya haiba ya Mji wa Zanzibar katika kipindi kifupi.
Alisisitiza kwamba ukamini wao katika kutoa huduma hizo ndio unaopelekea kuchaguliwa baada ya kushinda tenda dhidi ya Makampuni mengine Duniani na zaidi Barani Afrika.
“ Ujenzi wa baadhi ya Majengo ya Taasisi za Serikali , Mashirika ya Umma na hata miradi ya Jamii ni ushahidi uliowazi wa juhudi za Makampuni hayo”. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyahakikishia Makampuni yote yanayotowa huduma hapa Zanzibar kwamba Serikali itashirikiana nayo kwa lengo la kuhakikisha yanakamilisha miradi yao kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni hiyo ya Ujenzi wa Reli Nchini China Bwa Liu Rongyao alisema kwamba Ujumbe wao upo Nchini kukagua Miradi ya Ujenzi inayosimamiwa na Kampuni hiyo ikiwemo ile ya Makaazi ya Nyumba za Viongozi na Ofisi za Serikali .Ujenzi huo unafanywa kwa njia ya Mkopo kutoka Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.
Aidha Balozi Seif alikutana na Ujumbe wa Jumuiya inayojishughulisha na Miradi ya Maendeleo ya Kijamii kutoka Nchini Marekani ya Rosenthall Group.
Mwakilishi wa Jumuiya hiyo Bwana Robert Rosenthall alimueleza Balozi Seif kwamba Taasisi yao inaangalia taratibu za namna gani wanaweza kuelekeza nguvu zao katika Miradi ya Kijamii ndani ya Bara la Afrika.
Bw. Robert alisema mbali ya ujenzi wa nyumba katika kipindi kifupi unaofanywa na Taasisi yao lakini pia hutoa Taaluma ya huduma ya kwanza na Biashara mafunzo ambayo huchukua takriban Wanafunzi 150.
Naye Balozi Seif aliuomba Ujumbe huo kuangalia zaidi maeneo ambayo wanaweza kuwekeza hapa Zanzibar kwa nia ya kusaidia Uchumi wa Taifa.
Balozi Seif alisema yapo maeneo mengi yaliyopewa kipau mbele katika kuongeza kasi ya maendeleo akiyataja kuwa ni pamoja na Utalii, Kilimo, Huduma za Umme na Miundo mbinu.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikuwa na Maungumzo na Balozi wa Shirikisho la Ujerumani Nchini Tanzania Bwana Klaus Peter Brandes.
Bwana Peter alifika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar kumtambulisha rasmi Balozi Mdogo wa Shirikisho la Ujerumani atakayefanya kazi hapa Zanzibar Bwana Hans Dieter Allgaier.
Balozi Seif amemuahidi Bwana Allgaier kwamba Serikali itajitahidi kumpa mashirikiano zaidi ili kuona jukumu alilokabidhiwa na Nchi yake linafikiwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top