Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema suala la kuzingatia maadili ndani ya vyama vya Ushirika Nchini ndio njia ya msingi katika muelekeo wa mafanikio wa vyama hivyo .  
Balozi Seif alisema hayo mara baada ya  kuzindua   jengo Jipya  la Chama cha Ushirika cha Msingi Kata ya Makale Wilaya ya Manyoni Mkoani  Singida  mwishoni mwa ziara yake ya   siku tatu akiwa mlezi wa Mkoa huo  Kichama. 
Alisema uaminifu utakaoambatana na kuafanya kazi kwa pamoja miongoni mwa Wana ushirika  popote pale huchangia kupunguza ukali wa maisha pamoja na kujijengea hatma njema ya   kipato katika maisha yao ya baadaye. 
Balozi Seif alisema suala la Ushirika ni miongoni mwa  mambo yaliyozingatiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vile yanasaidia kuyakusanya makundi ya wana jamii kukaa pamoja katika kutatua matatizo yanayowakabili . 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Benki ya Maendeleo Vijijini Nchini Tanzania { CRDB } kwa mipango yake ya kusaidia kutoa mikopo kwa Vyama vya Ushirika . 
“ Hatua hii kwa kweli inaisaidia Serikali  kuwajengea mazingira bora Wana Jamii wake katika kujitefutia Maendeleo kupitia Vikundi vya Ushirika. Kwa mnasaba huu naahidi kuipigia Debe Benki Hii kwani hata mimi ni mteja wao wa zamani “. Alisisitiza Balozi Seif. 
Mapema akizpma risala kwa niaba ya wanachama wenzake wa chama cha Ushirika cha Msingi Makale katibu wa Ushirika huo Nd. Nassib Ali Juma Manyote alisema hadi sasa Chama chao kina Hisa  730 zenye thamani ya Shilingi Milioni 7,300,000/-. 
Nd. Manyote alisema chama hicho kinachojishughulisha na Kilimo cha zao la Tumbaku msimu huu uzalishaji ulifikia  Kilo laki 608,513 zenye thamani ya shilingi Bilioni moja , Milioni mia tatu na sabini na mbili, laki sita na 13 elfu. 
Katika hafla hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif aliahidi Kusaidia Kompyuta moja  na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Mh. Paul Luhanji akaahidi kusaidia Mashine ya uzalishaji wa Umeme unaotokana na Jua. 
Mapema Balozi Seif Ali Iddi aliitembelea  Ujenzi wa Jengo la  Skuli ya Sekondari ya Masista iliyopo Mitundu inayotarajia kuchukuwa wanafunzi 600 mchanganyiko. 
Mama Mkuu wa Shirika la Mama Huruma  Sister Verediana Hermani Alimueleza  Balozi Seif kwamba Skuli hiyo  imeanza na Wanafunzi wa Msingi   ambao wawazi wao huchangia ada kwa ajili ya kuendeleza Skuli hiyo. 
Sister Verediana alifahamisha kwamba  Uongozi wa Skuli hiyo pia husaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu na wale yatima kupatiwa Elimu bila ya ada. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameahidi kuchangia shilingi Milioni moja kwa ajili ya kusaidia uendelezaji wa Skuli hiyo  ambayo imekuwa ikifanya vizuri katika kutoa Wanafunzi bora Nchini Tanzania. 
Balozi Seif Akiwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi alikuwepo Mkoani Singida kwa Ziara ya siku tatu kuzindua miradi ya Maendeleo yakiwemo pia Majengo ya CCM Akiwamlezi wa Mkoa huo Kichama.
Othman Khamis             
Ofisi ya Makamu wa Pli wa Rais wa Zanzibar                     
                                                           

0 comments:

 
Top