Watendaji wa Sekta za Umma na hata zile za Kibinafsi wameombwa kusameheana endapo kuna makosa yaliyojitokeza ndani ya mwaka 2011 ili kujipanga vyema katika kupata ufanisi mkubwa zaidi kwenye mwaka unaoanza wa 2012.

Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika tafrija mahsusi aliyoiandaa kwa Watendaji wa Ofisi yake ya kuuaga mwaka 2011 na kuukaribisha mwaka 2012 iliyofanyika hapo nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema suala la ushirikiano ni vyema likazingatiwa na kuendelezwa mwaka ujao kwa mfumo wa kuona shida ya mmoja wao ni yao pamoja.
Alieleza faraja yake kutokanana na mfano waliouonyesha wa watendaji wake katika kuchapa kazi na utakuwa mfano kwa Wizara nyengine .
“ Kama kuna mtendaji ye yote hata kama Mkurugenzi niliwahi kumkera ndani ya mwaka uliopita naomba anisamehe. Hiyo ilikuwa ni kuona kazi za Serikali zinatekelezwa kwa umakini ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kukerwa kwake na baadhi ya Viongozi wanaopenda kuwa na tabia ya kunyanyasa Wafanyakazi wanaowaongoza.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Nchin Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Khalid Salum amesema ni jambo la faraja kula, kunywa na kucheza pamoja ikiashiria ushirikiano baina ya Viongozi na Wafanyakazi wao.
Dr. Khalid alisema hili ni tukio la Kihistoria na ni vyema likajengewa utaratibu wa kuendelezwa katika miaka ijayo.
Katibu Mkuu Khalid alifahamisha kwamba ni lazima kwa Watendaji kutathmini kasoro zilizojichomoza katika kipindi cha mwaka uliopita Kwa lengo la kujenga matumaini Bora zaidi ya mwaka ujao.
Tafrija hiyo iliyoshirikisha pia Baadhi ya Watendaji wa Wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitanguliwa na mlo ulioambatana na muziki laini wa Kisasa wa Rusha roho.
Mbali ya Rusha roho pia ilikuwepo ile ngoma Maarufu katika Visiwa vya Zanzibar inayocheza zaidi katika sherehe za harusi ya Beni { Maarufu Mbwa kachoka } kutoka kikundi mahiri cha Borafya.

0 comments:

 
Top