Serikali inafikiria kuagiza kutoka nje ya Nchi Wataalamu wa ushonaji wa nguo wenye uwezo wa kiwango cha juu kwa lengo la kufikia kuwa na Washoni wa fani hiyo katika ngazi ya Diploma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo kwenye mahafali ya tano ya chuo cha Ushonaji cha nguo wa Magomeni {Modern Tailoring Academy} zilizofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Sekondari ya Haile Selassie Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema mpango huo ukifikia hatua ya mafanikio utasaidia kupunguza matumizi ya fedha kutokana na uagizaji wa nguo zinazoshonwa nje ya Nchi kwa vile tayari uzalishaji wa mafundi wa ushoni utakuwa umeshaenea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikipongeza chuo cha Modern Tailoring Academy kwa kushirikiana na Serikali katika mipango yao ya kukuza ajira na kupunguza Umasikini.
Balozi Seif alisema mpango huo utawawezesha Vijana wanaopata mafunzo kama hayo kujiepusha na makundi maovu kwani muda wao watafikiria kuutumia katika kukabiliana na maisha yao ya kila siku.
“ Taaluma mnayoitoa huwasaidia Vijana kujiajiri wenyewe bila ya kutegemea ajira ya Serikali. Kwa kweli Chuo chenu ni muarubaini wa ajira kwa Vijana wa Zanzibar ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwataka Vijana waliomaliza mafunzo yao kufikiria njia ya kujiundia Vikundi vya Uzalishaji ili iwe rahisi kwa Serikali na Taasisi zake kuwapatia mikopo.
Balozi Seif aliwatahadharisha kuwa na Maadili na kufuata miiko ya kazi yao ambayo inahitaji mahaba na mapenzi kati yao na wateja watakaowahudumia.
Alisema tabia ya uongo kwa mafundi walio wengi hapa Nchini imeota mizizi hivyo ili wakubalike katika soko la ajira ambalo lina ushindani mkubwa watalazimika kujiepusha na tabia ya njoo kesho, njoo keshokutwa.
“ Kazi ya Ufundi ina Maadili na miiko yake, sasa mjuwe kwamba uongo usiokwisha ni adui mkubwa wa ufundi wa aina yoyote ile ”. Alitahadharisha Balozi Seif.
Katika Risala yao wahitimu hao wa Mafunzo ya Ushoni iliyosomwa na Nd. Issa Mohd Salum walitoa wito kwa Serikali kuandaa mazingira ya kuanzisha vyuo kama hivyo Wilayani ili Elimu ya Ufundi iwafikie wananchi aliowengi hasa Vijijini.
Wahitimu hao wameupongeza Uonozi wa Chuo hicho kwa kusaidia Jamii katika kupata muelekeo wa ajira.
Wamewaomba Wazazi Mitaani kuwapeleka watoto wao kupata Taaluma hiyo ambayo ni mkombozi katika maisha yao ya baadaye.
Walielezea faraja yao kuona pia Vijana wenye ulemavu na wale waliopata virusi vya Ukimwi wanapatiwa fursa hiyo kwa kupewa punguzo la asilimia 10% ya ada Chuoni hapo.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Modern Tailoring Academy Nd. Rashid Makame Shamsi amesema lengo la Chuo hicho ni Kuzisaidia Serikali zote mbili kupunguza wimbi la vijana wasiokuwa na ajira.
Nd. Rashid alisema katika kipindi kijacho uongozi wa Taasisi hiyo umefikiria kuwa na Mitandao ya Kompyuta kwa lengo la kutoa Taaluma inayokwenda na wakati Kimataifa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye ameahidi kuchangia Shilingi Milioni moja kusaidia chuo hicho cha Modern Tailoring Academy amekabidhi vyeti kwa Wahitimu mbali mbali waliomaliza mafunzo yao ya Madaraja tofauti.
Kati ya hao 231 ni wale wa Daraja la tatu, saba Daraja la Pili na kumi ni Daraja la kwanza.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top