Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kutekeleza kwa vitendo Mapendekezo yaliyomo ndani ya Ripoti ya Tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Sheni kuchunguza chanzo cha kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders mwezi Septemba Mwaka 2011.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kupokea Mchango wa Maafa uliotolewa na Uongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania hapo Zanzibar Beach Resort Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema Serikali haitamuonea haya mtu ye yote aliyehusika kufanya uzembe na kusababisha kuzama kwa Meli hiyo ambao umetajwa ndani ya Ripoti hiyo.
Makamu wa Poli wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Ripoti kamili iliyotolewa na Tume hiyo itawekwa hadharani muda si mrefu kupitia mitandao ya Internet ili kila Mwananchi apate fursa ya kuisoma kwa ukamilifu.
Mapema Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania Bw. Jumbe Menja alisema Uongozi wa Taasisi hiyo uliguswa na tukio hilo lililopelekea kuwa Historia hapa Zanzibar.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipokea sarafu ya shilingi 50,000/- iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania .
Sarafu hiyo aliyokabidhiwa Balozi Seif na Meneja wa BOT Tawi la Zanzibar Bw. Joseph Mhando iliambatana pia na kukabidhiwa kwa baadhi ya picha za kuchora za Viongozi wakuu wa Zanzibar.
Meneja Mhando alimueleza Balozi Seif kwamba Sarafu hiyo ni kwa ajili ya kumbu kubmu za Viongozi Wakuu na haitazunguuka katika mfumo wa Kibiashara.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top