Mchakato wa kupata katiba Mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania utakamilika vyema na kufanikiwa endapo Wananchi wa Tanzania wenye kufikia umri unaostahiki kutoa maoni kwa Tume itakayoundwa na Rais kuchukuwa maoni hayo watafanya hivyo wakati utapowadia.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika Mikutano tofauti ya wadi za Upenja na Kitope zilizomo ndani ya Jimbo lake wakati akizungumza na Viongozi wa CCM katika dhana ya kutoa taaluma ya kujiandaa na mchakato huo.
Balozi Seif ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wakati unakaribia wa kuhuisha Katiba Mpya katika kipindi cha miaka 50 ijayo kwa kuanza na mchakato huo.
Alifahamisha kwamba Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa Heshima kubwa kwa Wananchi kwa kuwataka kuanzisha Sheria kupitia Wabunge wao wa kupitisha utaratibu wa kuundwa kwa Tume ya kuratibu Maoni itakayoteuliwa na Rais hapo baadaye.
Balozi Seif alisisitiza kwamba lengo la mikutano inayoendelea hivi sasa ni kukumbushana namna ya kutumia fursa ya kutoa maoni muda utakapofika.
Hata hivyo Balozi Seif alikumbusha kwamba Jamuhuri ya Muungano itaendelea kuwepo kinachofafanulia ni mfumo wa aina gani ya Muungano watakaoutaka Wananchi waliowengi.
“ Katiba mpya tayari iwe imeshapatikana ifikapo mwaka 2014 baada ya zoezi zima la maoni, uundwaji na kukamilika kwake”.Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwakumbusha Wananchi kuelewa kwamba wao ndio wadau wakubwa wa Katiba ya Nchi. Hivyo mchango wao ni muhimu katika kuona suala la Katiba Mpya linakamilika vyema na kwa wakati uliokusudiwa.
Wakichangia kwenye Mkutano huo baadhi ya Viongozi hao wamependekeza kuwepo na Taaluma ya kutosha watakayopatiwa Wananchi kabla ya kufikia Maamuzi ya kutoa Maoni yao.
Wamesema hatua hiyo itatoa fursa ya Kidemokrasia ambayo itasaidia kuodosha mapema kasoro ambazo zinaweza kuleta manung’uniko kwa baadhi ya watu au makundi hapo baadaye.
Viongozi hao walieleza kuwa Wananchi walio wengi hawaielewi hata katiba iliyopo hivi sasa na wakashauri kupatiwa vipengele vinavyofaa kurekebishwa kwa ajili ya Katiba mpya.
Viongozi hao wameziomba Serikali zote mbili kuheshimu Maoni yanayotolewa na Umma kwa vile tayari wameshakuwa na uzoefu wa kuwagundua wajanja ambao hutumia nafasi ya ushawishi wakati wa utoaji wa Maoni ya Wananchi.
“ Wapo baadhi ya watu wanaobahatika kuteuliwa kuwa wajumbe wa kukusanya maoni katika Tume zilizopita ambao huonyesha ushabiki wao bila ya kujali kuzingatia Maadili ya Kazi waliyokabidhiwa na Umma ”. Alitahadharisha mmoja wa Viongozi hao waliochangia kwenye mkutano huo Bwana Khamis Hamad.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope ameelezea faraja yake kutokana na kuona muelekeo wa Chama chao umeeleweka vyema na Viongozi hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top