Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha Vijana kwamba huu si wakati wa mchezo katika suala zima la kujitafutia elimu kwa kujijengea maisha bora ya baadaye.
Balozi Seif alitoa tahadhari hiyo wakati akilizindua rasmi jengo jipya la Skuli ya Mkanyageni Wilaya ya Mkoani Pemba lililojengwa kwa nguvu za Wananchi wenyewe ikiwa ni shamra shamra za Maadhimisho ya Miaka 48 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.
Alisema Skuli ndio maisha yao ya baadaye.Hivyo tabia ya baadhi ya vijana kupenda utoro au anasa zisizokuwa na msingi haitawasaidia chochote.
Makamu wa Pili wa Rais alisisitiza kwamba Zanzibar inahitaji kuwa na Wataaamu wake na hilo halitafikiwa iwapo hakuta kuwa na nguvu za ziada za pande zote wakiwemo Wanafunzi wenyewe.
“ Kila mwanafunzi ni vyema akanuia kufikia elimu ya shahada ya kwanza ambayo itamjengea mazingira bora ya kuwa mkombozi wa Familia yake ”. Alifafanua Balozi Seif.
Aliwaomba Wazazi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuchangia huduma za elimu ili lile lengo la kila mwanafunzi kupatiwa haki ya elimu lifanikiwe licha ya kupanda kwa gharama za huduma hiyo za Elimu Kimataifa.
Balozi Seif amewapongeza wanafunzi wanawake hasa wa Skuli ya Mkanyageni kwa juhudi zao za kujikita zaidi katika fani ya Sayansi na hii ni changamoto kwa Wanafuzi Wanaume katika skuli hiyo.
Alisema hatua yao hiyo itasaidia kupunguza pengo kubwa liliopo la upungufu wa wataalamu wa fani ya Sayansi Nchini.
Balozi Seif ameelezea furaha yake kutokana na bahati waliyoipata Wananchi wa Jimbo la Mkanyageni ya kukamilishiwa Jengo lao hilo.
Alisema yapo majengo mengi ambayo bado hayajakamilishwa kwa utaratibu uliopo wa Wizara ya Elimu lakini hii waliyoipata wao ni baraka kwao.
Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban alisema Wizara hiyo inatarajia kuajiri Vijana waliomaliza masomo yao ya Chuo kikuu cha SUZA hivi karibu ili kusaidia kuziba upungufu uliopo katika maskuli mengi hasa ya Sekondari.
Waziri Shaaban alisema sambamba na hilo Wizara ya elimu inakusudia kujenga Skuli mpya ya Sekondari katika Jimbo la Mkanyageni kuanzia darasa la Tisa hadi la Kumi na Nne.
“ Tumefikiria kufungua Tawi la chuo kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA hapa Pemba. Lengo laWizara ni kuona wanafunzi Wanaomaliza Masomo yao ya Darasa la Kumi na Nne Wanaingia moja kwa moja Suza” Alisisitiza Waziri Shaaban.
Katika Risala yao Wananchi,wanafunzi na Walimu wa Skuli ya Mkanyageni wameelezea changa moto zinazowakabili skulini hapo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa Kompyuta, Foto kopi na uhaba wa Vikalio.
Katika kukabiliana na changamoto hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zazibar Balozi Seif Ali Iddi ameahidi kuchangia Kompyuta moja, wabunge na wawakilishi wa meneo hayo wakiwemo wale wa Viti Maalum akawataka kuchangia Mashine ya Foto Kopi.
Katika Mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni Mh. Mnyaa aliahidi kuchangia shilingi milioni tano kwa ajili ya ununuzi wa Vikalio vya darasa moja Skulini hapo.
Jengo Jipya la Skuli ya Mkanyageni limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 48,535850/- kati ya hizo Wananchi wenyewe wamechangia zaidi ya Shilingi Milioni 14.1 zilizobaki ni michango ya wahisani na nguvu za Serikali Kuu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top