Waumini wa Dini ya Kiislamu wameendelea kukumbushwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, hekima, busara na uaminifu ili kufikia kilele cha mafanikio katika maisha yao ya sasa na yale ya baadaye.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye Maulidi ya kumpongeza Rais Mstaafu wa Tanzania Shekh Ali Hassan Mwinyi kwa kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Falsafa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hapo Mtaa wa Msimbazi Mjini Dar es salaam.
Balozi Seif alisema Taasisi nyingi zikiwemo zile za Kidini zinakabiliwa na ukosefu wa uadilifu jambo ambalo huonekana kuwa kama la kawaida hivi sasa.
Alisema Jamii imekuwa ikishuhudia migogoro kadhaa isiyokwisha ndani ya baadhi ya Misikiti ambayo inayosababishwa na Viongozi waliokosa maadili hasa wakati inapotolewa misaada ambapo hujilimbikizia wao wachache.
‘‘ Ni jambo la kawaida siku hizi kushuhudia misaada inayotolewa kwa Waumini wote Misikitini kutumiwa na Waumini wachache na unapouliza misaada hiyo imekwenda wapi, siku ya pili utaamka sauti umekuganda ’’. Alisema Balozi Seif.
Makamu w Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza ShekhAli Hassan Mwinyi kwa Uongozi wake bora wa kupigiwa uliopelekea kushiba uadilifu na hatimae kutunukiwa Udaktari wa Falsafa.
‘‘ Ni nani katika sisi aliyekuwa tayari kuwajibika kwa sababu ya makosa yaliyotendwa na watu anaowaongoza ? Kwa Mzee Mwinyi hili haikuwa zito kwake kulifanya, na hii ilidhihirika katika miaka ya 70 alipokuwa Waziri wa Mambo ya ndani ’’. Alikumbusha Balozi Seif.
Alisema wakati wa uongozi wa Mzee Mwinyi Nchi ilitoka kwenye ukiritimba na kufungua milango ya kufanya Biashara kwa Mtanzania ye yote mwenye uwezo.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Uhuru alioutoa Mzee Mwinyi wa kufanya Biashara umewawezesha Watanzania kutosubiri tena Biashara ifanywe na wageni.
Mapema Mwenyekiti wa Umoja wa Wapenzi wa Mtume Muhammad {SAW} Sheikh Majid Saleh Mohd alimpongeza Shekh Ali Hassan Mwinyi kwa hekima na busara zake zilizompelekea kupata Heshima hiyo katika Jamii ya Watanzania.
Akitoa shukrani zake Rais Mstaafu wa Tanzania Shekh Ali Hassan Mwinyi ameelezea faraja aliyonayo kutokana na kutambua kwake upendo aliyoupata kutoka kwa Jamii iliyomzunguuka.
‘‘ Nimefurahi sana kwa mkusanyiko huu, nimemwagiwa sifa nyingi nashindwa kuelezea furaha niliyonayo ndani ya moyo wangu ’’. Alifafanua Shekhe Ali Hassan Mwinyi.
Katika hafla hiyo ya Maulidi Shekh Ali Hassan Mwinyi alikabidhiwa kofia maalum kama ishara ya upendo na kumbu kumbu kati yake na umoja wa Wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW }.
Pia Umoja huo ulikabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hati ya Uanachama wa Umoja huo pamoja na nishani Maalum ya ukumbusho wa kukubali kwake kuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya aina yake.
Maulidi hayo yaliyoshirikisha pia Wapenzi wa Mtume Muhammad { SAW } Kutoka Mombasa Nchini Kenya yameongozwa na Kasida zilizoghaniwa na Al -Madrasat Muhammadia ya Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top