Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuhakikisha kwamba utaratibu muafaka usioleta machungu unazingatiwa ili kuwapa faraja Wananchi walioathirika na upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Wananchi hao katika mkutano maalum wa kujadili mvutano uliojitokeza kati ya Wananchi hao na Uongozi wa Mamlaka ya ndege kuhusu upanuzi wa uwanja wa ndege ambao unalazimika nyumba na vipando vilivyomo katika eneo hilo viondolewe.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Karume Mbweni ulisimamiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Wananchi hao walisema mizozo mingi inaibuka kutokana na baadhi ya watendaji wa Serikali kutokuwa waadilifu kitendo ambacho kinawaondoshea imani.
Walisema tabia za baadhi ya watendaji kuchelewesha utaratibu wa ulipaji wa fidia katika awamu za mwanzo za upanuzi wa Uwanja huo zitasababisha ufukara unaoweza kuepukika.“ Hii ni Serikali yetu wenyewe kwa sababu walioko madarakani ni miongoni mwetu sisi. Hivyo ni vyema lile tunaloliomba kwa maslahi yetu na vizazi vyetu likazingatiwa ili kukinga mzozo ”. Alisema mmoja wa Wananchi hao Nd. Ramadhan Mrisho Rupia.
Wananchi hao walitahadharisha zaidi kuzingatiwa kwa hatma yao ya baadae ambayo ni muhimu katika maisha yao.
Akizungumza na Wananchi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali kamwe haikusudii kuwafanyia ubabe wananchi wake.
Balozi Seif alisema maamuzi ya Serikali wakati wote yanalenga katika kuona maendeleo yanaifikia Jamii yote ingawa baadhi yao wnaweza kuathirika na Hatua hizo.
“ Kama tunahitaji Maendeleo ni lazima inabidi tutumie rasilmali zetu wenyewe ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi hao kwamba malalamiko yao atayawasilisha katika ngazi za juu kwa lengo la kuzingatiwa zaidi.
Balozi Seif ameahidi kufuatilia malipo yote ya fidia ya Wananchi ambao hawajapatiwa katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa awamu zilizopita.
Hata hivyo makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Ardhi itaendelea kuwa mali ya Serikali kutokana na Historia ya Nchi hii ilivyokuwa.
Upanuzi huo wa Uwanja wa ndege wa Zanzibar una ukubwa wa Square Metre laki 928,268.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top