Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amekumbusha kwamba mafanikio ya kazi popote pale hupatikana na kuongezeka iwapo suala la kuheshimiana litapewa nafasi kubwa kati ya Viongozi na Watendaji wao.
Balozi Seif ametoa kumbusho hilo alipofanya ziara fupi ya kuangalia utendaji wa kazi na matatizo yanayokikabili Kituo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {Televisheni} Karume House Mjini Zanzibar.
Alisema utaratibu wa kujumuishwa kwa mawazo ya watendaji wadogo hata kama Dereva au Muhudumu unapelekea kuleta ufanisi wa haraka wa kazi katika Taasisi yoyote ile.
Balozi Seif alifahamisha kwamba nidhamu ya kazi lazima izingatiwe na kutekelezwa vyema vyenginevyo kazi inaweza kuharibika kama suala la dharau litaendelezwa miongoni mwa Watendaji na Viongozi.
“ Hakuna kitu ninachokichukia na kunikera ndani ya nafsi yangu kama tabia ya Wafanyakazi Hasa Viongozi kuwa na hulka ya kudhalilishana. Hii tabia ya Intimidation inanikera kweli kweli ”. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliwataka watendaji hao wa Kituo cha Matangazo ya Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } kuendelea kufanya kazi zao kwa uzalendo ili kuondoa mapungufu yaliyomo ndani ya uwezo wao.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali itajitahidi kuona yale yanayorekebishika yanatekelezwa mara moja kwa lengo la kukirejeshea hadi yake kituo hicho cha mwanzo cha rangi Barani Afrika.
“ Ni vyema Tv yetu ikarejea kama zamani na iwapo kama upo upungufu wa Wataalamu Suala hilo lishughulikiwe na Serikali ”. Alishauri Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Wakitoa malalamiko yao Baadhi ya Watendaji wa Kituo hicho cha matangazo ya Televisheni cha Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC } wameelezea kuzingatiwa kwa ufinyu wa Bajeti ya Vipindi ya kituo hicho.
Wamesema Bajeti hiyo haikidhi mahitaji halisi ya Utayarishaji vipindi na kulazimika kutumia Vipindi vingi vya kununua na vile vya kigeni ambavyo mara nyingi vinakiuka maadili na Utamaduni.
Kuhusu suala la Maposho ya ongezeko la muda wa kazi Watendaji hao wamesema jambo hilo ni ndoto na limekuwa likirejesha nyuma utendaji kazi wao wa kila siku.
Hata hivyo wameomba kupatiwa mafunzo ya mara kwa mara ili kujiweka tayari na mabadiliko ya mfumo wa kisasa wa Matangazo ya Digital unaotarajiwa kuanza rasmi mwaka 2015 Ulimwenguni kote.
Mapema akimkaguza Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif katika baadhi ya sehemu za Kituo hicho zikiwemo zile za Mitambo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar { ZBC } Nd. Hassan Abdulla Mitawi alisema hatua za awali zimeshachukuliwa na kituo hicho za kuelekea kwenye mfumo wa Digital.
Hata hivyo Nd. Mitawi alimueleza Balozi Seif kwamba Kituo hicho bado kinakabiliwa na changa moto ya Vifaa na Mafunzo ya Watendaji wake ili kujiweka tayari na mfumo huo mpya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif miongoni mwa sehemu alizobahatika kuzitembelea kituoni hapo ni pamoja na Chumba cha kurushia Matangazo { Master Contol Room } , Studio kubwa pamoja na Library.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top