MAONESHO ya sanaa ya kuadhimisha maridhiano ya kisiasa na kijamii Zanzibar, Jumamosi iliyopita yalihamia katika Uwanja wa Kisonge, ambapo vikundi vya Nadi Ikhwan Safaa (Unguja) na Juhudi Taarab kutoka Chake Chake, Pemba viliwapa uhondo mashabiki wengi waliojimwaga kiwanjani hapo.
Onesho hilo lililoandaliwa na taasisi ya Swahili Performing Arts Center, lilivutia wapenzi wengi sana kutokana na nyimbo murua zilizoporomoshwa na waimbaji magwiji wa vikundi hivyo viwili.
Kundi la Juhudi, ambalo lilikuwa la kwanza kupanda jukwaani, lilimudu vyema kuzikonga nyoyo za wananchi kwa nyimbo zao tamu kama vile 'Yatima' (Bi Asha Omar), 'Zimekwisha enzi zako' (Safia Abdalla), 'Mshikamano' (Rukia Issa) na 'Bora niombe' (Ali Said Wazera) uliowavutia wengi.
Nalo kundi la Nadi Ikhwan Safaa, klabu maarufu iliyotimiza miaka 106 mwaka huu, liliamsha hisia za hadhira iliyofurika uwanjani hapo, kwa nyimbo za 'Wadhanifu' (Sihaba Juma), 'Njangu' (Saada Mohammed) na 'Hakika nnakupenda' (Ally Massoud).
Vibao vingine vilivyowakosha wapenzi ni 'Naomba kwako bibiye'(Sameer Basalama),'Namuenzi' (Faudhia Abdullah), ambazo ziliwaibua washabiki kila mara katika viti vyao na kuungana pamoja kuserebuka.
Aidha wasanii wa vikundi hivyo kwa pamoja waliimba wimbo wa kusisitiza kuuendeleza maridhiano ya kisiasa na kijamii ya WaZanzibari, ukiwemo wimbo wa 'Maridhiano' (Malik Hamadi Wastara).
Katika mwendelezo wa onesho hilo, msanii wa siku nyingi Sihaba Juma, alirudi tena jukwaani kughani wimbo 'Nnazama', kabla ya Ali Said Wazera hajaonesha manjonjo yake katika wimbo 'Jibu la Moyo' na Saada Muhammed akahitimisha onesho hilo kwa kibao cha 'Leo tena'.
Katika kuwakumbusha malengi ya mradi wa 100% Zanzibari, Mkurugenzi Mtendaji wa Swahili Center alisisitiza umuhimu wa sanaa kuchangia katika kuimarisha misingi wa maridhiano na umoja wa kitaifa.
Tamasha hilo limepangwa kuendelea tena Jumamosi ijayo katika ukumbi wa Ngome Kongwe, ambapo kundi la ' Unguja Taarab All-Stars' na kikundi cha Mkota Ngoma kutoka Mkoani Pemba vinategemewa kutoa burdani mwanana.
Kufuatlia onsho hili itakuwa ni kilele cha mradi huu ambapo kutakuwa na maonesho ya siku nzima katika uwanja wa Gombani Pemba siku ya Jumamosi tarehe 3 Disemba 2011.
Mradi wa 100% Zanzibari umeandaliwa na taasisi ya Swahili Performing Arts Center kwa ushirikiano na Ubalozi wa Norway pamoja na kampuni ya mtandao wa simu wa Zantel.

0 comments:

 
Top