Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongezwa kwa hatua zake za dharura iliyochukuwa wakati wa kukabiliana na maafa yaliyosababishwa na Janga la Kuzama kwa Meli ya M.V Spice Islanders Mwezi Septemba mwaka huu.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mh. Leonidas Gama wakati wa kuwasilisha Mchango wa Shilingi Milioni 50,000,000/- uliotolewa na Wananchi ,Taasisi, Makampuni, pamoja na vyama vya siasa vilivyomo ndani ya Mkoa huo.
Mh. Gama amesema Wananchi wa Kilimanjaro wameeleza kufarajika kwao na juhudi hizo kufuatia harakati za uokozi ambazo kwa kiasi kikubwa walikuwa wazizifuatialia kupitia Vyombo mbali mbali vya Habari.
Alisema hatua hiyo ya uokozi iliyoambatana na Ziara za kuzifariji Familia zilizopatwa na maafa hayo imejenga historia nzuri upendo kwa Jamii ya Watanzania.
“ Inaridhisha kuona namna SMZ ilivyolishughulikia suala la uokozi pamoja na ziara za Viongozi Wakuu kuwafariji wafiwa katika Majimbo yao ”. Alisema Mh. Leonidas Gama.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Zanzibar Balozi Seif alisema Uongozi huo wa Mkoa wa Kilimanjaro wa kuja kufariji unaashiria kukugwa kwao na Msiba uliowapata Wananchi wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema kitendo hicho kinatoa picha halisi ya upendo na imani iliyoleta faraja kwa kwa pande hizo mbili za Muungano.
Wakati huo huo Balozi wa Finland Nchini Tanzania Bibi Sinikka Antila ametoa mkono wa pole kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kufuatia ajali ya Meli iliyotokea Mwezi Septemba mwaka huu.
Balozi Sinikka alisema licha ya kwamba ajali haiepukiki lakini Jamii inaweza kupunguza maafa iwapo itajipanga vyema.
Naye Balozi Seif katika mazungumzo hayo amewashauri Wafanyabiashara wa Finland kuangalia uwezekano wa kuingia ubia na wenzao wa Tanzania katika uwekezaji wa vyombo vya Baharini.
Balozi Seif alisema Sekta ya usafiri wa Baharini ni biashara pana na yenye faifa kubwa katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Othman Kahmis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

0 comments:

 
Top