TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameagiza kusitishwa mara moja shughuli zozote za ujenzi pamoja na miradi ya kiuchumi katika eneo la mikoko liliopo pembezoni mwa bahari Nyuma ya Afisi ya Baraza la Wawakilishi Mbweni nje Kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Agizo hilo la usitishwaji wa shughuli hizo litaendelea hadi itakapotolewa Ripoti rasmi ya Mamlaka za ardhi na Mazingira na kuwasilishwa kwa Makamu wa Pili wa Zanzibar baada ya uchunguzi wa Kimazingira utakapofanyika { Inviromental Impact ASSS }.
Balozi Seif Ametoa agizo hilo mbele ya Watendaji na Maafisa Wakuu wa Mamlaka za Ardhi, Mazingira na Misitu wakati alipotembelea ghafla eneo hilo mapema asubuhi.
Amesema ni vyema kwa eneo hilo la hifadhi ya mikoko likaachiliwa na kuendelea kubakia kama lilivyokusudiwa ili lisije likaleta maafa ya Kimazingira.
Balozi Seif amesisitiza kwamba Taratibu za Kimazingira lazima zifuatwe na kuwataka Watendaji wa Taasisi za Ardhi na Mazingira kutokubali kuburuzwa vyenginevyo Taifa linaweza kuwekwa pabaya Kimazingira.
“ Taratibu za Kimazingira lazima zieleweke na kufuatwa. Hichi ni Kisiwa . Tunakwenda wapi Jamani ? Hatuwezi kuachia mambo yakaenda hivi hivi ” Alikemea Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema uchafuzi wa mazingira katika baadhi ya maeneo ndani ya Visiwa vya Zanzibar inatishia, mfano wa hayo ni Kijiji cha Sipwese Kengeja Pemba na juhudi za dharura zinafaa kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo hilo.
“ Wakati Dunia Nzima Hivi sasa inazungumzia Suala la Kulinda na kutunza Mazingira sisi tunadharau na tunajisahau kama si Kisiwa ”.
Alisikitika Balozi Seif.
Ameziagiza Mamlaka za Ardhi, Mazingira pamoja na Misitu kushirikiana na kuwasiliana wakati yanapofikiwa maamuzi ya utolewaji wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa makaazi au Miradi ya kiuchumi.
Balozi Seif amesema Ushirikiano huo utasaidia kuondoa visingizio vya uvamizi holela wa maeneo hayo na pia kuepusha kwa asilimia kubwa uchafuzi wa mazingira.
Mapema Baadhi ya Watendaji Wakuu wa Taasisi hizo wamesema kwamba ufinyu wa Mashirikiano na Mawasiliano baina ya Taasisi hizo ndio unaopelekea kujichomoza kwa matatizo mbali mbali hasa yale ya ardhi hapa nchini.
Eneo la Hifadhi ya Mikoko la Mbweni liliopo nyuma na Afisi ya Baraza la Wawakilishi hivi sasa linaonekana.kuendelezwa ujenzi wa Majengo Tofauti pamoja na matayarisho ya kuendelezwa kwa Mradi wa Chumvi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top