TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kasi ya uwajibikaji unaoendelea kuonyeshwa na Wananchi wa Jimbo la Sichuan lilioko Kusini Magharibi ya China umepelekea eneo hilo kurejea katika haiba yake kufuatia kukumbwa na Tetemeko kubwa la ardhi mwaka 2008.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameeleza hayo wakati akihojiwa na Kituo cha Matangazo ya Televisheni cha Sichuan katika Hoteli ya Shangri-la Chengdu Nchini China baada ya kuutembelea eneo lililokumbwa na maafa hayo la Wenchuan Jimboni humo.
Balozi Seif amesema licha ya Mji huo kupata Janga lililopelekea watu 60,000 elfu kufariki Dunia na wengine 70,000 kupotea huku Majengo kadhaa kuharibika kabisa lakini haiba ya Mji huo imerejea tena na kupendeza.
Amewapongeza wananchi hao kwa kuharakisha kazi ya ujenzi mpya wa Mji huo katika kipindi kifupi cha miaka mitatu.
“ Mji ulivurugika kabisa katika kpindi kifipi cha tetemeko hilo lakini wananchi wa China kwa spidi yao wamefanikiwa kufanya kazi ya ziada kurejesha haiba ya Sichuan ”. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia suala la uwekezaji Balozi Seif alikiambia Kituo hicho cha Mtangazo ya Televisheni cha Sichuan kwa Tanzani bado imebarikiwa na utajiri wa mali ghafi, maeneo ya Utalii na sehemu za Uwekezaji.
Amewaomba wawekezaji wa China kuitumia fursa hiyo kwa wao tayari wameshapiga hatua kubwa katika sekta hizo na kuwahakikishia usalama wa Vitega uchumi vyao.
Balozi Seif amefahamisha kwamba hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na China.
“ Viongozi wetu wa mwanzo wakuu wa Mataifa haya Mwalimu Julius K. Nyerere wa Tanzania na Chairman Mao Tse Tung wa Jamuhuri ya Watu wa China tayari wameshatuwekea msingi imara wa Ushirikiano kati ya pande zetu mbili ”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif akiwa China Kuiwakilisha Tanzania katika Tamasha la Maonyesho ya Kibiashara na Viwanda ameipongeza China kupitia Jimbo la Sichuan kwa kutayarisha Maonyesho hayo yaliyoshirikisha Viongozi na Taasisi tofauti za Kimataifa.
Alisema hatua hiyo ni jambo zuri na lamfano linaloongeza kasi ya Maendeleo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top