PRESS RELEASE
Ujenzi wa Afisi za Wabunge ndani ya Majimbo ni uamuzi sahihi wa Bunge La Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha huduma za Wananchi zinapatikana kwa haraka muda wote. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope amesema hayo katika hafla fupi ya kukabidhiwa Afisi ya Jimbo hilo baada ya kukamilika Ujenzi wake.
Hati za Makabidhiano ya Afisi hiyo ya Mbunge wa Kitope imetiwa saini kati ya mbunge huyo Balozi Seif na Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini B Nd. Vuai Ali Vuai ambapo ujenzi wa Afisi za Wabunge unasimamia na Afisi za Wakuu wa Wilaya. Akikabidhi hati hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kakaskazini B Nd. Vuai Ali Vuai amesema ujenzi huo unafuatia azimio la bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania wa kujenga Afisi za Wabunge Majimboni.
Akipokea Afisi hiyo mbunge wa jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi amewahakikishia wananchi hao kwamba yeye na mwakilishi wa Jimbo hilo Mh. Makame Mshimba wataendelea kushirikiana na Wananchi hao ili Maendeleo ya haraka ndani ya Jimbo hilo yafikiwe. Wakati huo huo Balozi Seif Ali Iddi ameutembelea ushirika wa mwendo wa jongoo wa Kazole ambao unajishughulisha na ukulima wa mboga mboga.
Akiunga mkono juhudi za wanaushirika hao Balozi Seif Amekabidhi ndondo kwa kuendeleza ujenzi wa Afisi ya Tawi la CCM la Kijiji hicho pamoja na mpira wa Maji na vifaa vyake na kuahidi kutoa makalbi ya kisima ili kuwaondoshea shida ya upatikanaji wa maji katika mradi wao wa kilimo.
Balozi Seif pia amekabidhi msaada wa Matofali, Saruji, mchanga na fedha za fundi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Tawi la CCM La Kichungwani na kushauri ni vyema Tawi hilo likaanza kutoa huduma mwaka ujao.Vifaa na msaada huo kwa Kikundi cha Ushirika cha Uwendo wa Jongoo na Afisi za CCM vimegharimu Shilingi Milioni Moja Nukta Moja.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment