UCHUMI WA KIBEPARI CHANZO CHA MGOGORO WA MAFUTA
Kutangazwa punguzo la bei mpya za nishati ya mafuta tarehe 3/08/2011 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati (EWURA), ilipelekea makampuni ya mafuta kufanya mgomo baridi wa kutouza mafuta kwa siku kadhaa. Jambo lililowatia dhiki na mashaka raia na kudhoofisha maisha ya kijamii na kiuchumi, na hatimae EWURA kusitisha leseni ya kampuni ya BP kuuza mafuta kwa jumla kwa miezi mitatu, kampuni ambayo serikali inamiliki nusu ya hisa, na pia EWURA kuzionya kampuni nyengine za Camel na Engen.
Kwa kadhia hii, Hizb ut-Tahrir Afrika ya Mashariki ina haya ya kusema: Chanzo cha mgogoro huu ni upotofu wa nidhamu ya kiuchumi ya kibepari ambayo imechanganyikiwa ambako hudhihirika katika mambo matatu: Kwanza, kwa ajili ya maslahi haitofautishi baina ya ‘mali za binafsi’ na ‘mali ambazo ni za umma’ kimaumbile. Pili, utozaji wa makodi makubwa katika biashara, na mwisho unafiki wa dhana ya ‘soko huria’.
Nidhamu bora na tukufu ya kiuchumi ya kiislamu ambayo Hizb ut-Tahrir Afrika ya Mashariki inaamini kuwa ndio suluhisho pekee, imeweka mpaka wa wazi katika mafungu ya mali, kwa kuanisha ‘mali binafsi’ zinazoruhusiwa mtu yoyote kumiliki, ‘mali za serikali’ zinazofanana na mali binafsi isipokuwa tu humilikiwa na serikali kwa sababu ya kuhusika na haki ya jamii na ‘mali za umma’ ambazo huwa marufuku kumilikiwa na mtu binafsi kwa hali yoyote ile. Mali za umma kimaumbile ni za watu wote, kama vile mali zote za asili- migodi mikubwa ya maadini, fukwe, misitu, barabara na kila ambacho maumbile yake ni cha matumizi ya umma kwa ujumla wake. Mali hizi na mfano wa hizi huwa kamwe hazimilikiwi na mtu binafsi, taasisi au kikundi cha watu, kwa kuwa raia wataingizwa katika dhiki na mashaka kama haya yaliyojiri karibuni na yatakayoendelea kujiri chini ya mfumo huu. Pia hizi si mali za serikali kama ilivyo ndani ya mfumo potofu wa Ukomunisti, bali kazi ya serikali ni kuzisimamia tu na kuwafikishia umma kwa namna nyepesi ya haraka na muafaka. Mtume (SAW) alizuia kummilikisha Abyadh bin Hammal mgodi mkubwa wa chumvi, na pia anasema: “Watu ni washirika katika mambo matatu: maji, maeneo ya kulishia wanyama na moto.” Hapa ‘moto’ huhusisha kila aina ya nishati. Pia Uislamu ukaweka bayana kwamba kazi ya serikali ni kuwatumikia raia kama msimamizi na sio tu kutoza makodi, bali serikali nayo ijihusishe kuzalisha kwa kufanya biashara mbalimbali kama raia wengine. Na tatu, katika Uislamu hakuna unafiki wa kuchanganyikiwa kama ulivyo ubepari ambao asili yake huwapa mamlaka makubwa mabepari kuwanyonya wanyonge kwa dhana yao ya ‘soko huria’ na upande wa pili hujifanya ati una huruma kwa kupachika kiraka kinachogongana na mfumo wao kwa madai ya kiuwongo ya ati kuwasaidia wanyonge kwa kupanga baadhi ya bei za bidhaa muhimu! Ama Uislamu, ukiachilia mbali mali za umma na mali za serikali, mali zilizobakia zote ni haki ya raia wenyewe kupanga bei zao bila ya kuingiliwa, na hili pia huhusisha bei za huduma na mishahara kwa kuwa suala la kazi ni mkataba baina ya muajiri na muajiriwa peke yao. Na pale ambapo raia kapungukiwa katika kukidhi mahitaji yake ya msingi huwa ni jukumu la serikali (Khilafah) kumkidhia raia huyo mahitaji yake.
Hizb ut-Tahrir Afrika Mashariki inatangaza wazi kwamba kadhia hii ni dhihirisho nyongeza kwamba dunia leo inahitaji nidhamu mbadala ya kiuchumi kama inavyohitaji nidhamu mbadala ya kisiasa na kijamii ili kuokoa ubinaadamu, nidhamu ambayo ni ya kiislamu na sio nidhamu ya kibepari inayowatia watu dhiki na iliyosheheni viraka vinavyogongana na misingi ya mfumo wake.
Masoud Msellem
Naibu Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari
Hizb ut-Tahrir Afrika Mashariki

0 comments:

 
Top