Na,Jumbe Ismailly-Singida
MVUA kubwa zinazoendelea kunyesha Mkoani Singida zimeharibu zaidi ya ekari kumi za mashamba ya wakulima 30 wa Kijiji cha Mtipa,Manispaa ya Singida kufuatia maji kuanza kujaa kwenye mashamba hayo,hali inayoashiria kutishia maisha ya wakulima hao kukosa maeneo ya kulima.

Baadhi ya wananchi hao ambao maeneo ya mashamba yao yamechukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Singida kwa ajili ya kupisha mradi wa maji unaofadhiliwa na Benki ya dunia,ulioanza kujengwa tangu mwaka 2013.

Hata hivyo baadhi ya wamiliki wa mashamba hayo,Justina Jacobo Ntandu alifafanua kuwa pamoja na maeneo ya mashamba yao kuchukuliwa na serikali,lakini cha kushangaza hawajaanza kunufaika na mradi wa maji safi na salama kama ilivyokusudiwa na serikali.

“Wamekuja wakandarasi wetu wametuwekea mifereji,lakini mifereji hiyo sasa hivi wametuharibia na mashamba,maji hawajatengeneza sijui wamepotelea wapi”alihoji Justina.

Kwa mujibu wa mkazi huyo wa Mtaa wa Mwaghumpi,Kijiji cha Mtipa,eneo ilipowekwa mashine ya maji alikuwa akilitegemea kwa kilimo cha mazao ya chakula licha ya kuchukuliwa na serikali,hakuna kiasi chochote cha fedha alicholipwa kwa ajili ya fidia,zaidi ya kumharibia eneo lake ambalo kwa sasa linajaa maji kupita kiasi.

Naye Athumani Iddi ambaye pia ni mkazi wa Kijiji cha Mtipa alibainisha kuwa kutokana na mashamba yao kuchukuliwa kupisha mradi kuanzia mwaka jana hawakuwa na maeneo ya kulima na hata mwaka huu hawatakuwa na maeneo mazuri ya kuendeleza kilimo cha mazao ya chakula.

“Na mashamba hapa kama mwaka jana hatujalima,tulishindwa kulima kwa sababu maji yakija,mto huu umekatwa kwa sababu ile mito iliyokuwa inapita kuteremka kupita huko chini ukazuia yale maji yaliyokuwa yanafuata sehemu nyingine,yakafuata sehemu moja”alisisitiza mwananchi huyo.

Kwa mujibu wa mwanachi huyo awali maji hayo hayakuwa yakipitishwa kwenye mashamba lakini baada ya mitaro kuwekwa na kuelekezwa kwenye maeneo ya mashamba yao ndipo maji yalipoanza kusomba udongo kwenye mashamba na kuharibu utaratibu mzima wa kuendelea na kilimo cha mwaka uliopita.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Mtaa wa Mtipa mashariki Maulidi Selemani Mwangu alionyesha masikitiko yake kutokana na mashamba ya wananchi wa mtaa wake kuharibiwa na mafuriko ya maji yanayopita kwenye mashamba yao.

Hata hivyo mwenyekiti wa mradi wa maji wa Kijiji hicho,Msafiri Athumani Halimoja aliweka wazi kuwa mfereji uliowekwa bila kufukiwa na mkandarasi wa maji ulianza kutiririsha maji kwenye mashamba na kisha mashamba hayo kuanza kufukiwa na mchanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Joseph Mchina alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Mtipa,aliahidi kwamba katika kipindi kisichozidi wiki mbili atakuwa ameshughulikia kwa vitendo matatizo hayo na kuyamaliza kabisa badala ya kuongea kwa maneno tu.

“Kwa kweli naomba muda wa wiki mbili tu mje kuniona nitakuwa nimeshughulikia kwa vitendo malalamiko yote ya wananchi katika Manispaa,hususani ya miradi ya maji maana karibu yote ina matatizo,ikiongozwa na mradi wa Kijiji cha Kisaki”alisisitiza Mchina.

0 comments:

 
Top