Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmshauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amewanasihi Wananchi hasa Vijana wa Majimbo la Kisiwa cha Pemba kubadilika kwa lengo la kuachana na tabia ya kufanywa ngazi na baadhi ya Watu wakati wa uchaguzi na baadae kuamua kujinufaisha wao binafsi na familia zao.
Alisema miaka isiyopunguwa ishirini wananchi hao wamekuwa wakitumiwa kama vitega uchumi na watu ambao wamekuwa na hulka ya kuwakimbia mara tu baada ya kuwachagua.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akizungumza na Vijana wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Chake chake wakiwemo pia wale Vijana walioamua kuacha chama cha Wananchi { CUF } na kujiunga na CCM Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hifadhi Tibirinzi Chake Chake Pemba.
Alisema Wananchi na hasa Wanachama wa vyama vya siasa wana haki ya kubadilisha sera kwa kuamua kuhama chama ambacho wanahisi sera zake hazitekelezeki wala kuwaletea maendeleo yao.
Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Uchaguzi ya CCM Zanzibar alieleza kwamba watu wanaoufanya Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Ubunge wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ni ajira waelewe kwamba wanawaumiza Wananchi walioamua kuwachagua.
Alifahamisha kwamba kazi za Wabunge na Wawakilishi ni kuwatumikia Wananchi na ile tabia ya baadhi yao kutumia mafungu ya fedha za mafao yao kuanza kuhonga wananchi wakati unapokaribia uchaguzi ili wachaguliwe tena wafahamu kwamba wanafanya dhambi ambayo siku moja itawahukumu.
Aliwapongeza Vijana walioamua kuachana na vyama vya upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi chenye kujali na kuheshimu watu wenye dini, kabila na rangi tofauti.
Mapema Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Mama Asha Suleiman Iddi alisema mchezo unaochezwa na Wananchi hasa Vijana wa Majimbo ya Pemba wa kuwakubalia Viongozi wasiotimiza wajibu wao utaendelea kuwaathiri wenyewe.
Mama Asha alisema Viongozi hao wanachofanya baada ya kuchaguliwa na Wananchi ni kuelekeza nguvu zao katika kuimarisha maisha yao pamoja na kuwajengea hatma njema watoto wao binafsi kielimu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Vijana hao Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Tanzania { UVCCM } Shaka Hamdu Shaka alisema mabadiliko ya uongozi Pemba yanaweza kupatikana endapo Wananchi wenyewe wataamua kuyasimamia ipasavyo.
Shaka alisema mazingira ya ushindi wa CCM katika uchaguzi Mkuu unaokaribia katika nafasi zote za Uongozi Kuanzia Udiwani Hadi Rais ndani ya Kisiwa cha Unguja uko wazi na kinachosubiriwa kwa hivi sasa ni Tarehe ya kuapishwa kwa washindi hao.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment