Majeruhi 10 wanaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja kufuatia ajali tofauti walizopata wakati wakielekea kwenye mikutano ya Kampeni za uchaguzi inayoendelea katika sehemu mbali mbali hapa Nchini.

Ajali hizo takriban zote zimehusisha zaidi vijana waliokuwa wamepanda vyombo ambavyo vyengine vikiendeshwa kwa mwendo wa kasi na baadhi vilijaa idadi ya abiria kupindukia mpaka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata wasaa wa kufika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja kuwakagua majeruhi hao waliopata athari mbali mbali zikiwemo za kuvunjika viungo na michubuko.

Akiwafariji majeruhi hao kutoka Vyama vya Siasa vya CCM katika Mkutano wao wa Makunduchi na CUF katika Mkutano wao wa Nungwi Balozi Seif aliwatakia Vijana hao kupoa haraka na kurejea katika familia zao waendelee na harakati zao za Kimaisha.

Balozi Seif katika nasaha zake aliwaasa Vijana hao kuwa na tahadhari wakati wanapoendesha vyombo vya usafiri wa Bara barani kama gari na vespa kwani ni vyema wakaelewa kuwa mwendo wa kasi mbali ya kusababisha vifo lakini pia unachangia kuacha vilema vya maisha.

Naye Mkuu wa Kitengo cha kupokea wagonjwa wa dharura katika Hospitali Kuu ya Mnamo Mmoja Dr. Juma Salum Mbwana { Mambi } alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hali za wagonjwa hao zinaendelea vyema.

Dr Mambi alisema majeruhi waliotokana na ajali hizo wwengi kati yao tayari wamesharuhusiwa kurejea nyumbani baada ya kupatiwa huduma za Matibabu katika Hospitali hiyo.

Kampeni za uchaguzi zilizokuwa zikiendelea katika maeneo mbali mbali Nchini Tanzania zinatarajiwa kufikia kilele chake ifikapo Tarehe 24 Mwezi huu na uchaguzi Mkuu utafanyika Tarehe 25 zikiwa zimebakia siku tano.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top