Na,Jumbe Ismailly,Mkalama 
WANAFUNZI 706 wakiwemo wavulana 433 na wasichana 273 wa shule za msingi zilizopo Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Mkoani Singida wanatumia matundu 976 ya vyoo,hali inayohatarisha afya za wanafunzi hao.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Bravo Lyapembile alifafanua kwamba mahitaji ya matundu ya vyoo katika Halmashauri hiyo ni matundu 2,011 na kwamba mpaka sasa kuna jumla ya matundu 976 na hivyo kufanya upungufu wa matundu 135.

Aidha Lyapembile aliweka bayana pia kuwa sambamba na upungufu huo wa matundu ya vyoo,vile vile Halmashauri inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 501 kati ya mahitaji ya vyumba 1,056 huku kukiwa na vyumba 555 vya madarasa.

Kwa upande wa nyumba za walimu,mkurugenzi huyo alisema Halmashauri hiyo ina jumla ya nyumba za walimu 271 kati ya nyumba 706 zinazohitajika na hivyo kufanya upungufu wa nyumba za walimu 435.

Mkurugenzi mtendaji huyo aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa fupi ya maendeleo ya Halmashauri ya wilaya ya Mkalama kwa Naibu Waziri wa Elimu,Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa (TAMISEMI)Kassimu Majaliwa aliyekuwa na ziara ya siku moja wilayani hapa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Mkalama,Halmashauri hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawati 5,617 kati ya madawati 14,840 yanayohitajika licha ya kuwepo madawati 9,223.

Kuhusu ikama ya walimu,mkurugenzi mtendaji huyo alifafanua kuwa Halmashauri ya wilaya hiyo ina jumla ya walimu 706 wakiwemo wanaume 433 na wanawake 273 waliopo darasani na 17 waliopo ngazi ya kata na wilaya na hivyo kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo hivyo kuna upiungufu wa walimu 350.

Akizungumzia changamoto zinazoikabili Halmashauri,Lyapembile alizitaja baadhi kuwa ni pamoja na uhaba wa fedha za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia,ukosefu wa gari kwa ajili ya kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa taaluma katila shule za msingi na vituo vya MEMKWA.

Kwa upande wake afisa elimu wa wilaya Mwisungu Kigosi akitoa taarifa fupi ya shule ya msingi Munguli yenye wanafunzi 326 wakiwemo wavulana 157 na wasichana 169 alisema kuwa ina upungufu wa madawati 86 kati ya mahitaji ya madawati 109 na yaliyopo ni 23.

Kwa mujibu wa Kigosi shule ya Munguli yenye mradi wa bweni uliozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone jan,15,mwaka huu na kwamba kati ya wanafunzi 326 waliopo,wanafunzi 40 kati yao ni wa jamii ya kabila la wahadzabe,ambao kati yao wavulana ni 18 na wasichana ni 22.

Kuhusu matokeo ya mtihani wa taifa wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana,shule hiyo ilifanikiwa kufaulisha wanafunzi sita kati ya wanafunzi 21 waliofanya mtihani huo,ambapo shule ilishika nafasi ya kwanza kikata na nafasi ya 29 kati ya shule 79 zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Mkalama.

0 comments:

 
Top