Viongozi na Watendaji wa Chama cha Mapinduzi wana jukumu kubwa wanalopaswa kulisimamia katika kuwaelimisha Wananchi juu ya kuwachagua Viongozi wanaozingatia maadili, nidhamu pamoja na upendo wa kuwatumikia vizuri.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiyafunga mafunzo elekezi ya siku Tano yaliyoshirikisha Viongozi na watendaji wa CCM kuanzia ngazi ya Matawi hadi Mkoa wa Mjini yaliyofanyika katika Hoteli ya Dolfin Bay Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Balozi Seif alisema kuchaguwa Viongozi matapeli na wababaishaji ni tabia chafu ya kuipelekea jamii mazonge na matatizo yanayochangia kuvuruga mikakati na harakati zao za kujiletea maendeleo.
Alisema Tabia ya baadhi ya Viongozi pamoja na Watendaji wa Chama kuanzia ngazi ya Matawi hadi Mikoa ya kuwabeba mapema watu walioamuwa kuomba nafasi ya kugombea kuteuliwa kushika nyadhifa mbali mbali ni kwenda kinyume na Katiba pamoja na kanuni za Chama hicho.
Alitahadharisha kwamba Wanachama wa chama cha Mapinduzi hasa wakati huu wa kuelekea kwenye harakati za uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba lazima wasimame imara katika kukichunga chama chao kuvamiwa na watu wanaoangalia maslahi yao zaidi.
Aliwapongeza Viongozi hao kwa uamuzi wao wa kuandaa mafunzo hayo yenye lengo la kukihakikishia chama cha Mapiduzi kinaendelea kushika dola ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Balozi Seif alifahamisha kwamba mafunzo hayo elekezi yatasaidia kuamsha ari kwa Viongozi pamoja na Wanachama wao hasa ngazi ya chini kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi aliwahakikishia Viongozi na wanachama hao kwamba Sera na ilani ya CCM inayouzika na kutekelezeka ndio inayoleta ushindi na kuongoza dola tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya Siasa Nchini Tanzania.
“ Chama cha Mapinduzi kitahakikisha kinashika dola kutokana na udhaifu wa vyama vya upinzani kubeba doa katika azma yao ya kutaka wapewe ridhaa ya kuondoza Nchi “. Alifafanua Balozi Seif.
Akigusia suala la ada za Wanachama Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM aliwakumbusha Viongozi na watendaji wa Chama hicho hasa ngazi ya Matawi kuelewa kwamba wanalisimamia vyema suala hilo.
Alieleza kwamba ulipaji wa ada ya uanachama kwa wakati ndio njia pekee itakayokiwezesha Chama cha Mapinduzi kujiongezea mapato yatakayosaidia uendeshaji wa chama hicho.
Kuhusu katiba mpya iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba Balozi Seif aliwaagiza Viongozo wote wa Chama cha Mapinduzi kuendelea kuwaelimisha wanachama pamoja na Wananchi katika maeneo kuelewa katiba iliyopendekezwa ili iwe rasi kwao kutoa maamuzi wakati wa kura ya Maoni ukifika.
Alisema Katiba iliyopendekezwa na Bunge hilo ndio muarubaini pekee utakayoipatia tiba na njia Zanzibar kuondokana na kero ilizokuwa akizipigia kelele muda wote.
Alieleza kuwa suala la Mafuta na Gesi litakujakubakia kuwa Historia baada ya kutolewa katika orodha ya Mambo ya Muungano licha ya kwamba baadhi ya watu wanalishabikiwa wakisahau kwamba walikuwa mstari wa mbele kupinga Katiba iliyopendekezwa.
Akisoma maazimio ya washiriki hao wa mafunzo elekezi wa matawi hadi Mkoa wa Mjini Katibu wa UWT Wilaya ya Mjini Bibi Asha Mzee Khamis alisema washiriki hao wameazimia kuwadhibiti wanachama pamoja na viongozi wasio na maadili ambao kuachiwa kwao wanaweza kuzorotesha nguvu na utendaji wa chama hicho tawala.
Bibi Asha alisema washiriki hao wameamua suala la kusimamia maendeleo ya uchumi na ustawiwa jamii linapaswa kupewa msukumo ndani ya chama kwa lengo la kuwekeza katika kukijengea mazingira bora ya upatikanaji wa mapato ya uhakika chama hicho.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kufunga mafunzo hayo Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Ndugu Moh’d Omar Nyawenga alisema washiriki wa mafunzo hayo wamejipanga kuanzisha miradi ya kiuchumi ili kujenga uwezo wa utendaji ndani ya maeneo yao.
Mafunzo Hayo elekezi ya siku Tano yaliyowashirikisha Viongozi na watendaji 116 wa CCM kuanzia ngazi ya Matawi hadi Mkoa wa Mjini yalijumisha masomo 12 ambayo ni pamoja na kuhakikisha CCM Inaendelea kushika dola kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment