Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa msimamo wake wa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kusaidia Taalamu na uwezeshaji katika sekta mbali mbali za maendeleo na Kiuchumi Nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwaaga Madaktari Mabingwa wa China 21 waliomaliza muda wao wa kutoa huduma za Afya Zanzibar na kuwakaribisha wapya 21 walioingia Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita kushika nafasi hizo.

Maagano na makaribisho hayo ambayo yaliambatana na chakula cha mchana alichowaandalia Madaktari Mabingwa hao wa Kichina yamefanyika nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema Jamuhuri ya Watu wa china imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo nchi hiyo ilianza kuleta timu ya Madaktari bingwa wa afya kufanya kazi Zanzibar kuanzia mwaka 1965.

Alisema timu za madaktari hao wa China zimekuwa zikifanya kazi kubwa za kutoa huduma za afya licha ya baadhi ya wakati kufanyakazi katika mazingira magumu jambo ambalo limeleta faraja na upendo kwa wananchi wanaopata fursa ya kuhudumiwa na Madaktari hao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Madaktari hao Mabingwa wa China walioambatana na Balozi wao Mdogo hapa Zanzibar Bwana Xie Yun Liang kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya afya kutokana na umuhimu wake wa kulinda na kustawisha afya za Wananchi wake.

Alisema kipaumbele hicho ni pamoja na kuimarisha miundo mbinu katika ujenzi wa vituo vya afya sambamba na vile vinavyoanzishwa na Wananchi wenyewe vinavyokadiriwa kupatikana katika umbali usiozidi Kilomita Tano.

Naye Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa China Bwana Xie Yun Liang aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Nchi hiyo itaendelea kusaidia maendeleo ya Zanzibar katika lengo lake la kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili uliodumu kwa zaidi ya miaka Hamsini sasa.

Balozi Xie alisema mkazo pamoja na mipango itaendelea kuimarishwa katika kuona China inazidisha nguvu zake za misaada katika Sekta za Afya, Elimu pamoja na miundombinu ya huduma za maji, kilimo na mawasiliano.

Mapema Kiongozi wa Madaktari wa China waliomaliza muda wao wa kazi wa miaka miwili Zanzibar Dr. Liu Yaping kwa niaba ya wenzake alisema wanajivunia ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa wenyeji wao ambao umewajengea nguvu za kufanya kazi kwa ari.

Dr. Liu Yaping alifahamisha kwamba kazi ya afya inahitaji uvumilivu mkubwa unaoibua upendo mkubwa na kusaidia kuleta ushirikiano kati ya Daktari na Mgonjwa na hatimae kuzaa udugu kati ya wahusika hao wawili.

Kiongozi huyo wa Madaktari Bingwa wa China waliomaliza muda wao ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Afya Zanzibar kwa msaada mkubwa ulioipa Timu yake katika muda wao wote wa miaka miwili waliokuwepo hapa Zanzibar.

Timu Mpya ya Madaktari Bingwa 21 kutoka Jamuhuri ya Watu wa China inayoongozwa na Dr. Xu Zhuo Qun itakuwepo Zanzibar kutoa huduma za Afya ambapo miongoni mwao Madaktari 12 watafanya kazi Unguja na 9 Kisiwani Pemba.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top