Matayarisho ya awali ya maandalizi ya ujenzi wa Kiwanja cha Michezo cha Mao Tse tung kiliopo Mperani Kikwajuni Mjini Zanzibar yameanza rasmi kwa hatua ya utafiti wa uchunguzi wa udongo wa eneo hilo.

Mhandisi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Mbarouk alieleza hayo wakati akimpatia ufafanuzi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefanya ziara fupi ya kuangalia matayarisho hayo.

Mhandisi Ali Mbaouk alimueleza Balozi Seif kwamba utafiti huo wa udongo unaofanywa kwa kuchukuwa aina tofauti za udongo kwenye vishimo 34 vinavyochimbwa ndani ya eneo la uwanja huo unatarajiwa kuchukuwa muda wa siku 20.

Alisema udongo huo utafanyia utafiti wa kina na wataalamu waliobobea ambao kukamilikwa kwake watatoa ripoti kamili itakayofuatiwa na utangazaji wa tenda kwa Makampuni yatayokuwa tayari kujenga uwanja huo.

Alifahamisha kwamba ujenzi kamili wa uwanja wa Mao Tse Tung unatarajiwa kuanza rasmi mwezi wa Febuari mwaka 2016 chini ya ufadhili wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.

Akitoa ufafanuzi wa Ramani ya ujenzi wa uwanja huo Mhandisi Ali Barouk alimueleza Balozi Seif kwamba uwanja huo utakapomalizika utakuwa na Viwanja viwili vya mchezo wa soka, kimoja kitakachokidhi michezo ya Pete pamoja na Kikapu.

Alieleza kwamba lipo eneo litakalotengwa maalum kwa michezo mbali mbali ya ndani { INDO GAMES }, Majukwaa ya watazamaji eneo la watu Maarufu { VIP } pamoja na ofisi za watendaji wa uwanja huo.

Akielezea furaha yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kukamilika kwa uwanja wa huo wa Mao Tse Tung kutasaidia kuupunguzia mzigo mkubwa uwanja wa michezo wa Amani.

Balozi Seif alisema uwanja wa Amani kwa sasa ndio pekee unaobeba michezo yote ya Kimataifa na Kitaifa ,Sherehe tofauti ikiwemo ile kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na matamasha mbali mbali.






Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top