Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba nguvu, kauli na mshikamano wa pamoja kati ya Wazee,Viongozi na Wanachama wa CCM wa Jimbo la Nungwi unahitajika ili Jimbo hilo lirejee kusimamiwa na CCM yenye nguvu, sera na Ilani zinazotekelezeka.
Alisema mshikamano wa wahusika hao kwa kushirikiana na Wananchi ndio fursa pekee wanayoweza kuitumia wakati wa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia katika kuwachagua Watu waadilifu na waungwana watakaofaa kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza na Wazee waasisi na Viongozi wa CCM Jimbo la Nungwi hapo katika Ukumbi wa CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni Balozi Seif Ali Iddi alisema haki ya kidemokrasia inampa fursa kila mwanachama wa cha chama cha Siasa mwenye sifa zinazokubalika kugombea Uongozi lakini ni vyema jamii inayomzunguuka mtu huyo ionyeshe nia sahihi ya kumuunga mkono.
Balozi Seif alifahamisha kwamba wakati wa umimi katika kugombea nafasi za Uongozi umekwisha kwani tabia hiyo imekuwa ikileta usumbufu miongoni mwa wananchi pamoja na kukipunguzia nguvu za uwajibikaji Chama cha Mapinduzi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi alitahadharisha kwamba tabia ya makundi ndani ya chama hicho ni hatari hasa wakati Taifa linakaribia kuingia katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.
Alieleza kwamba Wanachama wa chama hicho ni vyema wakazingatia mtu anayekubalika na kundi kubwa la wanachama miongoni mwao pamoja na Jamii ya Wananchi wa sehemu husika ili kuepusha mgawanyiko usio wa lazima.
“ Huyu wangu katika Demokrasia ndio mwanzo wa vurugu na makundi. Kama walio wengi hawakubaliani na wako utalazimika kuikubali demokrasia ya wengi katika uteuzi au uchaguzi huo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Balozi Seif amnbae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba ipo miradi mingi ya maendeleo na kijamii iliyoanzishwa na Viongozi waliopita katika baadhi ya Majimbo lakini hukosa kuendelezwa kwa sababu ya Viongozi wapya wanaoongoza kwenye majimbo hayo wametofautiana itikadi za siasa.
Alisema kuwa tabia hiyo mbaya ndani ya jamii iliyopo hivi sasa inawanyima haki ya kupata huduma za msingi Wananchi katika miradi ya kijamii kama vile afya, elimu na maji safi na salama.
Naye Mke wa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Mama Asha Suleiman Iddi aliwakumbusha Wazee na Viongozi hao wa Jimbo la Nungwi kwamba Uzalendo ndani ya Uongozi lazima upewe msukumo mkubwa unaostahiki katika kufanikisha majukumu ya Taifa.
Mama Asha aliwataka Wazee na Viongozi hao kuhakikisha kwamba changamoto na matatizo yanayokwaza utendaji wao wanapaswa kuyawasilisha kwa Uongozi wa juu ili yachukuliwe hatua zinazostahiki.
Mapema Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd. Haji Juma Haji alieleza kuwa heshima ya Chama cha Mapinduzi ndani ya Jimbo la Nungwi itaimarika iwapo Viongozi na wanachama wa CCM Jimbo hilo watadumisha mshikamano wao.
Nd. Haji Juma alisema udhaifu uliotokea kwenye uchaguzi wa Jimbo hilo mwaka 2010 utafutika na kutorejea tena endapo makundi hayo mawili yataondoa migongano yao inayotokea kutokana na maeneo wanayotoka.
Wakitoa maoni na michango yao katika Mkutano huo Baadhi ya Wazee na Viongozi wa CCM Jimbo la Nungwi wameonya kwamba tabia ya baadhi ya viongozi kuendekeza tamaa ya fedha hasa kipindi cha uchaguzi ndiyo inayoleta migogoro kati yao na Wanachama wanaowaongoza.
Walisema suala la kufuatwa kwa maadili pamoja na kutolewa elimu ya Demokrasia linapaswa kupewa kipa umbele na pande hizo kwa lengo la kupunguza au kuondosha tabia hiyo inayodhoofisha nguvu za Chama.
Wazee na Viongozi hao wa Jimbo la Nungwi waliuomba Uongozi wa Juu wa Chama pamoja na Serikali kuendelea kuwa na utaratibu wa kufanya ziara za mara kwa mara katika wilaya na Majimbo ili kujuwa changamoto zinazowakabili wanachama na Wananchi wa maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Walisema yapo matatizo na changamoto zinazoweza kuungwa mkono na Viongozi hao katika ziara zao na kuwapa nguvu na ari wananchi hao kuzidi kutekeleza malengo waliyojipangia kila siku.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment