Na: Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewasisitiza waislamu nchini kuachana na tabia ya kugombania misikiti, kwani haisaidii kuendeleza dini hiyo.
Amesema misikiti ni nyumba za Mwenyezi Mungu, hivyo hakuna sababu kwa waislamu kulumbana kwa sababu za kugombea uongozi au kutokana na tofauti ya kimadhehebu.
Maalim Seif ametoa nasaha hizo wakati akifungua msikiti wa Ijumaa MASJIDIL AQSAA katika kijiji cha Kiboje Mkwajuni, Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema Uislamu ni dini yenye nidhamu kamili, na kuwataka waumini wa dini hiyo kufuata nidhamu hizo katika kuendesha mambo yao bila ya kukaribisha malumbano na mifarakano baina yao.
Amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuuimarisha na kuuendeleza msikiti huo kwa kuendeleza harakati za darsa, sambamba na kuwaandalia watoto muda wa kutosha kuweza kuhudhuria katika darsa hizo ili kuwajenga kimaadili.
Amesema madrasa zina mchango wa kipekee katika kuwaandaa watoto na kuwakuza kuwa raia wema walioleleka katika maadili ya Kiislamu, na kwamba waislamu bado wana jukumu la kuzianzisha madrasa kwa wingi na kuhakikisha kuwa watoto wanapita katika darsa hizo kupata malezi sahihi.
Amefahamisha kuwa hivi sasa Zanzibar inahitaji malezi mazuri kwa watoto na vijana kuliko wakati mwengine wowote, kutokana na matishio makubwa yanayojitokeza na kuvurugika kwa maadili mema.
Amewakumbusha waislamu kuchangia harakati za dini hiyo kwa kujenga na kuimarisha misikiti na madrasa, kwani kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wake katika kuziendeleza nyumba hizo za Mwenyezi Mungu.
Aidha Maalim Seif amewakumbusha waislamu kuendeleza umoja, maelewano, na mshikamano miongoni mwao, na kujiepusha na chuki miongoni mwa waumini wa dini hiyo na dini nyengine.
Amesema serikali imefanya juhudi kubwa kuiwezesha jamii kuondokana na hasama, chuki na kudharauliana na badala yake kujenga mazingira ya umoja, mshikamano na maelewano, mambo ambayo yanapaswa kuungwa mkono kwa vitendo.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa waangalifu katika kuwachagulia vyuo vijana wao, ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa maadili .
Amesema baadhi ya vyuo hasa vilivyoko nje ya nchi havina misingi mizuri ya malezi, na kwamba bila ya kuwa waangalifu jamii inaweza kupoteza wengi ambao hatimaye wanaweza kujitumbukiza katika vitendo viovu.
“Chagueni vyuo vitakavyo wanufaisha vijana, sio kijana kwa sababu anakwenda kusoma nje ya nchi umkubalie tu, wazazi na walezi ni lazima mufuatilie kujua uhakika wa vyuo hivyo” alisisitiza.
Akizungumza kabla ya hotuba ya Ijumaa, Sheikh Thabit Noman Jombo kutoka ofisi ya Mufti wa Zanzibar amewahimiza waislamu wa eneo hilo kuutumia msikiti huo kama sehemu ya kutolea taaluma.
Amesema Zanzibar ilikuwa kitovu cha elimu katika nchi za Afrika Mashariki, na hakuna budi kuienzi historia hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mapema akisoma risala ya wazee wa msikiti huo Sheikh Abdalla Rajab, amewashukuru waliojenga msikiti huo mkubwa katika kijiji chao, na kuahidi kuutunza na kuweka darsa ambazo zitakuwa endelevu.
Amesema uwepo wa msikiti huo ni faraja kwa wanakijiji na maeneo jirani, kwani pia wameweza kuondokana na shida ya maji safi na salama iliyokuwa ikiwakabili kwa kipindi kirefu.
0 comments:
Post a Comment