Na: Khamis Haji, OMKR.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itatoa mashirikiano makubwa kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kukabiliana na maradhi mbali mbali na kuimarisha afya za wananchi wa Zanzibar.

Maalim Seif ametoa ahadi hiyo alipokuwa na mazungumzo na Mwakilishi mpya wa WHO hapa Zanzibar, Dk. Andemichoel Ghirmoy aliyekwenda kujitambulisha huko ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema wananchi wenye afya bora ndio wenye nafasi kubwa ya kujiletea mafanikio na kukuza maendeleo ya nchi yao, hivyo Serikali itaunga mkono mipango na Sera zote za kuimarisha afya za wananchi.

Amesema Shirika hilo lina mchango wa kipekee kwa Serikali na wananchi wa Zanzibar kutokana na mashirikiano mazuri yaliyopo kati yake na Zanzibar na ameahidi mashirikiano hayo yatazidi kuimarishwa kwa faida ya wananchi.

Naye Mwakilishi huyo wa WHO alisema Shrika hilo litaendeleza mipango mbali mbali iliyokwisha anzishwa, ikiwemo kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya akinamama na watoto, kutokomeza maradhi ya kichocho na kusaidia vita dhidi ya maambukizi ya ukimwi.

Dk. Ghirmoy amesema Zanzibar imeweza kujipatia sifa kubwa katika kutokomeza maradhi ya Malaria na kwamba WHO litakuwa bega kwa bega na Serikali kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelezwa.

Amewataka wananchi wa Zanzibar kuacha kubweteka kutokana na mafanikio hayo na badala yake waongeze kasi ya mapambano ili kuhakikisha kuwa kasi ya maambukizi ya ukimwi inazidi kupungua.

0 comments:

 
Top