Mwanamichezo Maarufu Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza Hassanali alisema Kampuni yake ya Hassan and Son’s inakusudia kuanzisha mpango maalum wa kuzisaidia timu za Maskuli Unguja na Pemba ili ile ari na vugu vugu la michezo lirejee kama zamani.

Raza alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi Seti za jezi, soksi na mipira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya Timu ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi iliyofanyika Ofisini kwa Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar pia ilihudhuriwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Moh’d pamoja na Viongozi wa Timu ya Wizara hiyo.

Raza alisema wakati umefika kwa washirika wa michezo Nchini kuunga mkono mpango huo wa kurejesha mashindano ya mara kwa mara katika maskuli ya Zanzibar kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na timu imara zitakazokuwa na uwezo wa Kimataifa.

Akipokea msaada huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimpongeza Mwanamichezo huyo Maarufu wa Zanzibar Moh’d Raza kwa jitihada zake za kuunga mkono sekta ya Michezo hapa Nchini.

Alisema kitendo cha Mwanamichezo huyo ni miongoni mwa uzalendo aliouonyesha ambao unastahiki kuigwa na washirika pamoja na wanamichezo wengine.

Balozi Seif alisema juhudi za Mwanamichezo huyo zilipelekea kuteuliwa kuwa mshauri wa Rais anayesimamia michezo pamoja na kuwa Mwenyekiti wa Saidia Zanzibar Ishinde { SAZI } katika awamu zilizopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambalo limo ndani ya Ilani ya chama cha Mapinduzi ni kukuza michezo hapa Nchini.

Alishauri Taasisi zinazosimamia michezo Nchini kwa kushirikiana na Ofisi yake ziandae utaratibu wa kuanzisha Ligi Maalum za Mawizara ya Serikali na tayari Mwanamichezo Moh’d Raza ameonyesha nia shauku ya kuzisaidia Timu hizo kwa kuzipatia vifaa endapo ligi hiyo itaasisiwa rasmi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top